Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za wakati huu ndugu yangu katika Kristo, bila shaka umefanikiwa kutimiza ahadi kadhaa ulizojiahidi kuzitimiza siku ya leo.
Nyakati ambazo huwa hatuna kitu mfukoni huwa tuna unyenyekevu mkubwa sana, kwa wale ambao tunajua wanaweza kutusaidia kile tunahitaji kwao. Hali hizi za kutokuwa na uwezo wa kifedha umeficha uhalisia mkubwa sana kwa wengi wetu.
Unaweza kumwona mtu ni mpole na mnyenyekevu, kumbe huo sio uhalisia wake, subiri apate uwezo wa kifedha ndio utamwona alivyo na vituko vya ajabu.
Unaweza kumwona mfanyakazi mwenzako ni mnyenyekevu na mtu mwema mwenye kujali wengine, kumbe anafanya hivyo tu kwa sababu ya malengo fulani. Akishakuwa juu yenu kwa kuanza kuwaongoza, unaona ule unyenyekevu wake wakati bado yupo chini, unatoweka kabisa na kuanza kuwafanyia mambo ya ajabuajabu.
Unaweza kumwona mtumishi wa Mungu akiwa bado yupo kwenye hali fulani ya chini, anakuwa na unyenyekevu mzuri sana. Ila Mungu akishamwinua zaidi, anaanza dharau na kuona yeye ndio yeye, anasahau kabisa kule alipotolewa na Mungu.
Hizi tabia za hivi huwa zinamkwaza sana Mungu, lazima tulielewe hili na kuliweka moyoni, ili linapotokea tatizo tusianze kumlaumu mtu yeyote. Wakati sisi wenyewe ndio tumesababisha matatizo yatutokee.
Unakuta mtu kabla hajapata ajira alikuwa na mahusiano mazuri na wazazi wake, lakini baada ya kupata kazi. Anakuwa hana tena muda na wazazi wake, wakati anatafuta kazi wazazi wake walichangia sehemu kubwa ya yeye kufanikisha mipango yake. Wanaweza kuwa hawakushiriki sana sehemu kubwa sana lakini wakawa walihusika vizuri kuhakikisha anakula chakula.
Unakuta mwanaume wakati hana kazi nzuri ya kueleweka, alikuwa na heshima kubwa sana kwa mke wake. Ila baada ya kupata kazi nzuri ya kueleweka, au biashara zake zikaanza kumwendea vizuri na kumpa faida nzuri. Utamwona akianza kumletea mke wake vituko vya ajabu, mara hivi mara vile.
Unakuta mwanamke wakati hana uchumi wa kwake binafsi wa kujitengemea, alikuwa na heshima kwa mume wake. Ila baada ya Mungu kumwinua akaanza kupata pesa za kutosha, na akawa na uhakika wa kufanya mambo yake. Utamwona akianza kuleta dharau kwa mume wake, na kumwambia utanitisha nini kama pesa ninazo.
Nakueleza vitu halisi unavyokutana navyo kila siku, ni vitu vinavyofanywa na watu wenye akili timamu kabisa. Nakwambia unaweza usimwelewe sana mtu tabia yake wakati yupo kwenye hali ya chini, utamwelewa vizuri pale akaunti yake ya bank itakapokuwa inasoma mamilion ya pesa.
Kumbe nafasi ambazo tunazipata, zingefaa sana kufanya vitu vizuri Zaidi vya kumtukuza Mungu wetu. Kumbe nia ya Mungu kukubariki ukapata pesa nyingi zaidi, ni ili uwe baraka kwa familia yako, na sio mwimba.
Mungu kukupandisha viwango fulani vya juu kiroho, ni ili uwe msaada kwa wale ambao wapo chini, na sio kuwa sehemu ya kuonyesha majivuno/majigambo ya kutaka kupewa sifa wewe badala ya Mungu.
Tunaweza kumtazama zaidi mfalme Rehoboamu aliyezisahau na kuziacha njia za Mungu baada ya kufanikiwa kwake kuwa mtawala.
Rejea: Ikawa ulipothibitika ufalme wa Rehoboamu, naye amepata nguvu, aliiacha torati ya BWANA, na Israeli wote pamoja naye. 2 NYA. 12:1 SUV.
Baadaye tunaona hasira ya Mungu ikiwaka juu yake na Israel wote, kwa kuziacha sheria za Mungu wao.
Rejea: Ndipo akaja Shemaya nabii kwa Rehoboamu, na kwa wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu kwa sababu ya Shishaki, akawaambia, BWANA asema hivi, Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo nami nimewaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.2 NYA. 12:5 SUV.
Baadaye tunaona baada ya kugundua kuwa wamekosa mbele za MUNGU waliamua kwenda mbele za Mungu kwa toba. Hawakusubiri muda mwingine wa kujadili, maadamu waligundua kosa lao wakatubu mbele za Mungu, naye Mungu akawasamehe.
Rejea: Ndipo wakajinyenyekeza wakuu wa Israeli na mfalme; wakasema, BWANA ndiye mwenye haki. Naye BWANA alipoona ya kwamba wamejinyenyekeza, neno la BWANA likamjia Shemaya, kusema, Wamejinyenyekeza; sitawaharibu; lakini nitawapa wokovu punde, wala ghadhabu yangu haitamwagika juu ya Yerusalemu kwa mkono wa Shishaki. 2 NYA. 12:6-7 SUV.
Vizuri sana kugundua pale ulipokosa ukaenda moja kwa moja mbele za Mungu kutubia lile kosa. Vyema ukijua ulipowakosea watu, unaenda kuwaomba msamaha na sio kuwaonea aibu na kuwakwepa.
Pamoja na wakuu wa Israel na mfalme wao kujinyenyekeza mbele za Mungu, bado tunamwona mfalme Rehoboam akiendelea kujinyenyekeza zaidi mbele za Mungu kwa kosa alilofanya.
Rejea: Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa BWANA, wakaja walinzi wakazichukua, wakazirudisha tena chumbani mwa walinzi. Naye alipojinyenyekeza, ghadhabu ya BWANA ikamgeukia mbali, asimharibu kabisa; tena yalionekana katika Yuda mambo mema. 2 NYA. 12:11-12 SUV.
Napenda uondoke na picha hii, yapo mambo tunafanya kwa sababu ya uchanga wa kiroho, ila tunapokua kiroho, tukagundua makosa yetu. Vyema kutubu na kuachana mara moja na tabia za kitoto zinazoondoa mahusiano yetu na Mungu.
Jifunze Neno la Mungu maisha yako yote, penda kujifunza kwa watumishi wa Mungu mbalimbali waliofanikiwa. Kujifunza hakuna mwisho, kufanya hivyo utajengeka maeneo mengi sana kiroho na kimwili.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
www.chapeotz.com