
Uongo umeonekana ni silaha nzuri sana ya kuwaumiza wengine wasiojiweza kujitetea kwa jambo fulani. Ama kuwachafua wale waliofanikiwa kwenye maeneo mbalimbali katika maisha yao.
Kuonekana hivyo uongo umekuwa ni sehemu ya maisha ya watu, wapo watu wasio na nia njema kwa wengine. Wamekuwa wakitumia uongo kama silaha yao ya kuwaangamiza.
Wapo watu wametumia uongo kuharibu nafasi za kazi za wenzao, wapo watu wametumia uongo kusambaratisha ndoa za wenzao, wapo watu wametumia uongo kuharibu mahusiano mazuri baina ya mtu na mtu.
Kuna watu wameufanya uongo ni sehemu ya maisha yao, mambo wanayoyafanya huwezi kuamini kabisa vile unamwona mtu alivyo na maneno ambayo anayatengeneza kwa wengine.
Sasa leo napenda kukuonyesha vile uongo ulivyo na madhara makubwa kwa mtu ambaye anautumia uongo kuharibu nafasi za wengine au kuharibu maisha ya watu.
Rejea: Shahidi mdhalimu akimwinukia mtu ye yote na kushuhudia juu yake ya upotoe; ndipo wale watu washindanao kwa mambo yale na wasimame wote wawili mbele za BWANA, mbele ya makuhani na waamuzi watakaokuwapo siku hizo; nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye; ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. KUM. 19:16-19 SUV.
Ikiwa mtu anatumika kama shahidi wa uongo, yaani kumsemea mtu mabaya ambayo hakusika nayo kuyafanya. Katika agano la kale ilikuwa sharti afanyiwe vile alitaka mwenzake afanyiwe, kama ni kuua alitakiwa auwawe yeye.
Leo sisi hatuna nafasi hiyo ya kumuua yule mtu ambaye ameonekana alichokuwa anasema juu ya mtu mwingine ni uongo.
Kwanini hatuna nafasi hiyo? Siku hizi kisasi ni juu ya Bwana, ikiwa kisasi ni juu ya Bwana. Uwe na uhakika Bwana atafanya vile alivyosema yeye.
Rejea: Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. RUM. 12:19 SUV.
Naweza kusema kama ulikuwa unataka kumlipiza mtu kisasi kwa yale aliyokutendea, unaweza usitoe adhabu inayostahili kwake. Kwahiyo Mungu akataka umwachie yeye hiyo kazi alipe, na Mungu kulipa mwenyewe ujue haitakuwa adhabu ndogo.
Shahidi wa uongo au kusema uongo juu ya mwingine, imesemwa sana madhara yake yatakayompata yule anayeusema huo uongo.
Rejea: Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uongo ataangamia. MIT. 19:9 SUV.
Anayesema uongo juu ya mwingine anaweza asione sana madhara siku hiyo hiyo ya kile alikuwa anafanya, ila nikuhakikishie hili, yapo madhara makubwa sana kwa msema uongo.
Yale yale aliyoyatengeneza yeye yamwangamize mtu mwingine, ama yamfukuzishe kazi mwingine, ama yamgombanishe na mkuu wake wa kazi, ama yamgombanishe na mke/mume wake.
Yatamrudia kwa namna ambayo itakuwa mbaya zaidi kwake, yale mashimo aliyoyachimba kwa ajili ya wengine wadumbukie humo ndani. Ndiyo mashimo yale yale atakayodumbukia yeye mwenyewe.
Rejea: Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danielii, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. DAN. 6:24 SUV.
Ipo mifano mingi sana ndani ya Biblia Takatifu juu ya wale waliowasemea wengine uongo, wale waliofanya vitu kwa hila. Madhara yake yaliwarudia wao wenyewe.
Nakusihi sana kama umekuwa shahidi wa uongo kwa wengine, yaani unatoa habari za uongo kwa wengine ili waharibikiwe. Kabla hasira ya Mungu haijatenda kazi kwako, tubu na usirudie tena hiyo tabia mbaya.
Unaweza kusema huyu naye anasema nini, unaweza kufikiri hivyo ila ukisubiri kisasi cha Bwana. Utakuwa umeingia hasara mbaya sana, ni bora kwenda mbele za Mungu kutubu naye atakusamehe.
Uongo haufai kabisa katika maisha yetu, hasa sisi ambao tumeokoka, jilinde sana na hili. Unaweza ukapata faida ya hapa duniani kwa muda mfupi kwa uongo wako, ila fahamu hutofika mbali na hiyo faida yako.
Yesu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma neno la Mungu kila siku, napenda nikukaribishe kwenye kundi hili la wasap. Tuma ujumbe wako wasap kwa namba +255759808081.