Asifiwe Yesu Kristo, habari za wakati huu. Nikualike katika somo hili tuwe pamoja katika kujifunza, karibu sana.
Ukishatangaza umeokoka na ukaonekana umesimama katika kweli ya Mungu, na ukaonekana una msaada mkubwa wa kiroho kwa jamii. Ukawa balozi mzuri wa Kristo, kila mahali ukifika lazima jina la Yesu Kristo liinuliwe kupitia wewe.
Ujue watu watakutazama kwa jicho lingine kabisa, hata pale unapotoa ushauri wako juu ya utata wa jambo fulani watu wanakusikiliza na kupata kuchukua ushauri wako. Maana ndani yako yupo Roho wa Mungu anayekutumia wewe kuwasaidia wengine.
Habari zako zinaweza kuenea kwa wengi sana hata kama wakiambiana wao kwa wao bila wewe kusikia. Ila fahamu mtu wa Mungu yeyote aliyesimama na Mungu vizuri ujue sifa zake kila mtu anayemzunguka atakuwa nazo. Hata kama unaona watu hawasemi sana na wewe, jua wanasemezana wao kwa wao.
Ndio maana ilifika kipindi Yesu Kristo akauliza wanafunzi wake, mataifa wanamsemaje huko nje, Yesu alitaka kujua ni jinsi gani wanamchukuliaje huko nje. Ni nzuri pia wakati mwingine ukajua watu wanakuchukuliaje katika huduma yako, ili kama kuna jambo unaenda ndivyo sivyo uweze kuliboresha zaidi. Pia unapaswa kufahamu kila mmoja aliyesimama vizuri na Mungu wake kuna misemo mingi sana juu yake.
Usikae hapo ukafikiri watu hawakujui vizuri, watu wanakuelewa kuzidi hata unavyodhani wewe japo sio kwa mambo yote. Hata kama unawaona kama vile hawakufahamu, sifa zako wanazo vizuri sana.
Watu wakishakujua wewe ni mwalimu na mshauri mzuri katika eneo fulani la maisha ya kiroho au kimwili, ujue watakutumia vizuri sana na watapenda kujua mafanikio na maendeleo yako.
Pamoja na kuwa hodari katika hayo yote, inafika kipindi unafikwa na wewe na jambo gumu, jambo ambalo watu wataanza kupata mashaka na wewe. Wapo watakaosema ulikuwa humtumikii Mungu wa kweli, na wapo watakaosema umemtenda Mungu dhambi ndio maana yamekukuta hayo.
Pamoja na kukuona kama wanavyokuona wao na kukutafsiri wao wajuavyo, bado wapo watakaoogopa kukuuliza kimetokea nini mpaka upatwe na tatizo la namna hiyo. Na wapo watakaopata ujasiri wa kukuuliza.
Kweli inafika wakati unaenda kumsalimia rafiki yako, ukimwangalia jinsi anavyoteseka unakosa hata neno la kumwambia. Hata ile pole uliyotaka kumpa unaona kama vile haina maana sana kwake kwa wakati huo, kwa jinsi alivyo na hali mbaya.
Upo wakati unafika hata ule ushujaa wetu wa kuwasaidia wengine kwa kuwaombea na kuwashauri mambo mbalimbali ya maisha yao kiroho na kimwili unapotea. Inapofika kwetu hata ule ujasiri tuliokuwa nao mwanzo unapotea kabisa kutokana na kusongwa vitu vizito kwetu.
Hata wale waliotuamini kuwa tunaye Mungu wa kweli ndani yetu, wataanza kupata mashaka na kuhisi haikuwa kweli kabisa. Pamoja na kupata mashaka hayo, wapo watakaopata ujasiri kukuuliza na wapo watakaobaki na kusemea maneno ya pembeni.
Haya tunajifunza zaidi kwa Ayubu aliyekuwa mtu wa Mungu, na mtu aliyetegemewa na jamii kuwa ni mtu aliyesimama na Mungu vizuri. Ila alipofika kwenye majaribu mazito, marafiki zake walianza kupata wasiwasi wa Ayubu atakuwa amemsokosea Mungu wake. Maana hata yeye Ayubu alifedheheshwa moyo wake kwa mateso anayopitia.
Rejea; Mtu akijaribu kuzungumza nawe, je! Utaona ni vibaya? Lakini ni nani awezaye kujizuia asinene? Tazama, wewe umewafunza watu wengi, Nawe umeitia nguvu mikono iliyokuwa minyonge. Maneno yako yamemtegemeza huyo aliyekuwa anaanguka, Nawe umeyaimarisha magoti manyonge. Lakini sasa haya yamekufikilia wewe, nawe wafa moyo; Yamekugusa, nawe wafadhaika. Je! Dini yako siyo mataraja yako, Na matumaini yako si huo uelekevu wa njia zako? Kumbuka, tafadhali, ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? Au hao waelekevu, walikatiliwa mbali wapi? Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, Na kupanda madhara, huvuna yayo hayo. Kwa pumzi za Mungu huangamia. Na kwa kuvuma kwa hasira zake humalizika. AYU. 4:2-9 SUV.
Huyu ni Elifazi ananena na Ayubu maneno haya, anajaribu kumweleza ushujaa wake, huku akimchomekea maneno ya kuuchoma moyo wake. Maana Elifazi anavyojua yeye mtu akiwa na hali kama yake atakuwa amemkosea Mungu.
Inatufunza nini hii; hapa tunajifunza unapaswa kusimama na Mungu wako vizuri, wakati wa shida yako kila mmoja ataongea lake, kila mmoja atajifanya anakufahamu sana hata lililokupata limekupata kwa sababu fulani. Wakati hata wewe mhusika unayepitia magumu hayo hujapewa taarifa na Mungu wako, ila kwa wakati wako wa kujaribiwa watasema mengi.
Mwisho wa yote utapaswa kusimama wewe kama wewe, na Mungu wako, hata kama unatapitia maumivu makali kiasi gani. Bado unapaswa kutambua uweza wa Mungu maishani mwako, hii imani ya kuelewa haya inategenezwa sasa na bidii yako ya kujifunza Neno la Mungu.
Viatu vingine ni vigumu kuvivaa, maana vinakuwa vya moto kweli ndani yake kutokana na jambo gumu unalopitia wakati huo. Lakini fahamu Mungu alijua unao uwezo wa kuvivaa ndio maana ameruhusu hayo yakupate, haijalishi hicho kiatu hakivaliki kwa wengine kwako kitavalika hata kama kinaumiza.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kujifunza haya.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.