
“Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo?” Mt 11:7 SUV.
Wakati Yesu aliposema kwamba Yohana siyo “unyasi ukitikiswa na upepo”, alikuwa akimaanisha kuwa tabia ya haki ya Yohana na sifa yake ya kama mhubiri aliyekataa kabisa kukana alichokuwa anaamini. Alikuwa mtu imara aliyesimamia imani yake bila kuyumbishwa yeyote.
Yohana alihubiri amri za Mungu pasipo shaka yeyote wala hakuwaogopa wengine watamfanya nini au watajisikiaje, wala hakufuata mkumbo wa wale watu waliokuwa wanaoogopa kuisema kweli ya Mungu.
Dhambi ya Herode haikuguswa kabisa na mamlaka yote ya Kiyahudi, lakini Yohana hakukaa kimya hata kidogo, aliendelea kuhubiri Injili ya nguvu. Kuwataka watu waache njia zao mbaya na wamwelekee Mungu.
Yohana alikuwa kinyume kabisa na dhambi alisimama kama mwamba imara akionesha uaminifu wake thabiti kwa Mungu wake na kwa Neno lake.
Alisimama pamoja na Mungu dhidi ya kukemea dhambi bila kuogopa, kuhakikisha anatenda sawasawa na neno la Mungu linavyomtaka afanye au atende, ijapokuwa ilimgharimu maisha yake kuisema kweli ya Mungu.
“Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye”, Mt 14:3-4 SUV.
Kila mhubiri wa neno la Mungu anapaswa kujiangalia kwa kujithamini juu ya utumishi wake, maana Kristo ataipima kazi au huduma ya kila mmoja wetu.
Sio hilo tu, tabia ya kila mmoja na msimamo wake dhidi ya dhambi ikoje, tunapaswa kujua kuwa siku ya mwisho kila mmoja atapimwa alisimama vipi katika hayo yaliyo kinyume na Mungu.
“Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa”, Lk 1:17 SUV.
Ikiwa Yohana na mitume wengine waliweza kusimama imara, nasi tunapaswa kuwa imara katika imani, hatupaswi kuogopa kukemea dhambi kwa nguvu zetu zote bila kujalisha tutamkwaza nani.
Elewa hatuhubiri maneno ya watu, tunahubiri neno la Mungu, ukilihubiri neno la Mungu kama lilivyo haitakuwa na shida, na hutakuwa na hatia mbele za Mungu. Utakuwa umetimiza wajibu wako kama mwana wa Mungu au kama mtumishi wa Mungu.
Simama imara katika imani thabiti ya Yesu Kristo, usiyumbishwe na dunia hii, iseme kweli, kemea dhambi, watu wamjue Yesu Kristo, hata kama watakataa unachowaambia, wewe utakuwa umeifanya kazi yako au utakuwa umetimiza wajibu wako.
Unapaswa kujawa na nguvu za Roho Mtakatifiu na neno la Mungu, ndipo utaweza kunena neno la Mungu kwa ujasiri na usahihi. Hili sio jambo la kununua dukani, unahitaji kumwomba Mungu akujaze Roho Mtakatifu, na unapaswa kusoma neno la Mungu.
Mwisho, karibu kwenye kundi la wasap la kusoma biblia kila siku na kutafakari, ukihitaji kujiunga na kundi hili, wasiliana nasi kwa wasap +255759808081, utaunganishwa.
Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest