“Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu”, 2 The 3:6 SUV.
Watu wasio na utaratibu waliosemwa hapa ni wale watu waliokuwa wanazurura na hawakupenda kufanya kazi.
Walichokuwa wanafanya ni kuwa walitumia vibaya ukarimu wa kanisa na walipokea misaada mbalimbali kwa wale watu waliokuwa wanajishughulisha kufanya kazi.
Mtume Paulo anatoa agizo la kujitenga na watu wa namna hii wasiopenda kufanya kazi, wale wanaosubiri wengine wawajibike ndio wanaenda kuomba wasaidiwe.
Hakuzuia kutoa msaada kwa wahitaji, wale waliokuwa wanastahili msaada kweli walipaswa kusaidiwa.
Wale ambao walikuwa vizuri, hawakuwa na tatizo lolote la kiafya, wala hawakuwa walemavu wa kushindwa kufanya kazi, walipaswa kufanya kazi.
Tofauti na hapo wote ambao tupo vizuri na tunaojiweza kimwili tunapaswa kujishughulisha kuhakikisha tunapata mahitaji yetu ya kimwili.
Mtume Paulo anawakumbusha kuwa hakutegemea kila kitu kwao japo alikuwa anaweza kufanya hivyo, alijishughulisha kuhakikisha mambo mengine yanaenda.
“Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote”, 2 The 3:7-8 SUV.
Watu wanaokushauri usifanye kazi sana kwa sababu umeokoka, watu hao hawafai kuwa marafiki na hupaswi kuwasikiliza.
Ukiambatana na mvivu na akawa rafiki yako wa karibu kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa hiyo roho mbaya ya uvivu.
Bora kuwa na ukaribu naye kwa mkakati maalumu wa kumsaidia na urafiki huo uwe na mipaka tofauti na urafiki wa jumla.
Mungu wetu ni mchapa kazi mzuri, ukiwa unasema unamwamini Mungu alafu ni mvivu, mtu usiyependa kujituma kwenye kazi ujue umevamiwa na roho zisizotakiwa kwako.
Kuokoka hakutuzuii kufanya kazi kwa bidii, kuwa mtumishi hakukufanyi uwe unalala tu bila kujishughulisha na kazi za mikono, fanya kazi kadri ya nafasi yako.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest