“Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri”, Mwa 34:1‭-‬2 SUV.

Yakobo alipokuwa anatoka kwa Labani alipewa maagizo na Mungu arudi nyumbani kwao kwa Isaka, Lakini badala yake aliweka makazi kwenye mji wa kipagani wa shekemu.

Kinyume kabisa na Mungu alivyomwamuru kwenda kwa baba yake Isaka, ambayo ilikuwa ni nchi yao walikozaliwa.

“Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa”, Mwa 31:13 SUV.

“Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako”, Mwa 35:1 SUV.

Mambo aliyokutana nayo hasa kwa binti yake Dina kubakwa, ilimfanya ajutie kwa uchungu mwingi uchaguzi wake mbaya.

Baada ya tukio hilo kwa binti yake, na vijana wake kwenda kuua, aliamua kurudi Betheli mahali ambapo aliamriwa awali na Mungu aende, aliharibu miungu yote ya kigeni nyumbani kwake.

“Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu”, Mwa 35:2 SUV.

Kipi tunajifunza kupitia kisa hiki cha kutisha? Lipo jambo la muhimu sana la kujifunza katika maisha yetu ya wokovu.

Mungu hutupa maelekezo muhimu ya kufanya, huwa hatufuati vile anatuelekeza, badala yake huwa tunafuata mawazo yetu. Matokeo yake tunapata matatizo kwenye maamuzi tuliyofanya.

Yapo maelekezo mengi sana ndani ya neno la Mungu, ambayo Mungu anatutaka tuenende katika njia anayoitaka yeye.

Tunapoenda kinyume na vile anatutaka, madhara yake huwa makubwa sana katika maisha yetu. Tunaingia kwenye shida ambazo hazikuwa lazima kuingia humo.

Tunaweza kusema kwenda kinyume na maagizo ya Mungu ni kulazimisha kuingia kwenye matatizo kwa nguvu, matatizo ambayo hutupa majuto makubwa katika maisha yetu.

Binti wa Yakobo aliingia kwenye shida ya kubakwa kwa sababu aliweka makazi kwenye mji wa kipagani, mji ambao ulikuwa hauna hofu yeyote ya Mungu.

Hatupaswi kujiingiza kwenye majuto yasiyo ya lazima, tufuate maelekezo ya Mungu anayotupa kupitia neno lake au watumishi wake.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081