Naendelea kuelewa vizuri kuwa Neno la Mungu ni hazina kubwa sana, iliyobeba mambo mazito na mengi sana yamhusuyo mwanadamu.
Nimechukua nusu saa kusoma sura hii ya 10 katika kitabu cha Mhubiri, nimejaribu kulinganisha maneno haya kwa kusoma biblia nne zenye viswahili tofauti.
Nimefanya hivi baada ya kuona kuna vitu vizito ambavyo sikuvijua vizuri mwanzo, yaani leo nilikuwa napata darasa jipya kabisa kuhusu eneo hili ninaloenda kukushirikisha hapa.
Unapoambiwa Neno la Mungu limebeba maisha ya mtu, usiwe na mashaka kuhusu hili. Unaweza usielewe sana ila elewa Mungu alimaliza kabisa kila kitu, maarifa yote sahihi alituwekea ndani ya biblia.
Upo wakati watawala/viongozi wetu wa kazi, hututupia maneno ya hasira na kuumiza mioyo yetu. Maneno ambayo hutufanya tuone wametudharau na kutushushia heshima zetu.
Tunapoona hivyo mara nyingi huwa tunakimbilia kujiuzulu nafasi zetu tulizokuwa nazo. Bila kupata muda wa kutulia kwanza, ndipo tufanye maamzi yaliyo sahihi.
Kweli inaumiza hasa mtu mzima unapotupiwa maneno ya kejeli na kuumiza moyo wako. Pamoja na hayo usiwe na haraka kujiuzulu nafasi uliyokuwepo.
Ndio wewe ni mtu mzima, na huyo anayokuambia maneno ya kuumiza moyo wako ni mtoto mdogo. Ila amekuzidi cheo, tulia kwanza usiache kazi kwa sababu yake.
Wakati mwingine unaweza kufanya kosa kweli, ukakemewa haswa, usiwe na haraka kujiuzulu. Jinyenyekeze, kupitia unyenyekevu wako ukasababisha kufuta makosa yako.
Walioko jeshini watakuwa wananielewa vizuri hili ninalowaeleza hapa. Jeshini ni cheo, mzee wa miaka 50, anaweza kukemewa na kuamrishwa na kijana wa miaka 30, tena anaweza kupewa adhabu mbele ya vijana wadogo kabisa.
Hata makazini kwetu pia yapo, unaweza kuletewa boss mtoto yaani mwenye kufanana umri na mwanao hata watatu kumzaa. Akakukemea haswa kutokana na kosa ulilofanya, na wewe kwa hasira ukaona ujiuzulu nafasi yako.
Neno la Mungu linatueleza wazi kabisa, tusifanye hivyo tunapokasirikiwa na wakuu wetu. Chukua muda kujenga utulivu, unyenyekevu hubadilisha hata yale maamzi ambayo yalipagwa kutokea kwako.
Rejea: Mtawala akikuwakia hasira, usijiuzulu; makosa makubwa huweza kufutwa ukiwa mnyenyekevu. Mhubiri 10:4 BHN
Nimeipenda hii biblia ya habari njema, ina kiswahili kinachoeleweka zaidi. Ni kiswahili ambacho kila mtu anaweza kukielewa kirahisi sana, nimeona vyema kuitumia ili uweze kuelewa vizuri zaidi.
Bila shaka umeona andiko hilo, usiwe na hasira za karibu kufanya maamzi. Maana hasira hukaa kifuani mwa mpumbavu.
Rejea: Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu. Mhubiri 7:9 SUV.
Ili kuendelea kupata masomo mbalimbali kupitia email yako, jiunge na mtandao wetu kwa kuweka email yako. Pia unaweza kuungana nasi group la whatsApp la kusoma Neno la Mungu kila siku, tumia namba za whatsApp hapo chini kuwasiliana nasi.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081