Yapo mambo Mungu anaweza kukutendea katika maisha yako, ukashindwa kujizuia kabisa. Badala yake unaanza kumwaga machozi ya furaha kuu ndani ya moyo wako na nje ya macho yako kwa kile Mungu alichokutendea.
Unaweza kuona mwenzako analialia nini, lakini ukifuatilia kwa umakini unaona Kwa kweli huyu mtu anastahili kutoa machozi.
Inaweza ikawa kero kwa wengine kwa kutokujua kwao vizuri kile Mungu amemtendea mtu yule. Pia unaweza ukaambiwa kilichomfanya alie usichukulie ule uzito wa ndani kabisa, kutokana na hujawahi kupatwa na jambo kama lile.
Unaweza kumshangaa mtu anatoa shukrani mbele za Mungu huku analia kwa kupata mtoto, huwezi kujua amehangaika miaka mingapi akitafuta mtoto yule, pia huwezi kujua amenusurika vipi kumpoteza yule mtoto na uhai wake.
Unaweza kumshangaa mtu akitoa shukrani huku machozi yakimtiririka kwa kupata mke/mume, huwezi kujua gharama aliyotoa mbele za Mungu. Kumwomba ampatie mke/mume mwema, huwezi kujua hapo alipo ana miaka 40 lakini hajawahi kuolewa/kuoa.
Huwezi kujua mama yule anayetoa machozi mengi kumshukuru MUNGU kumpa mume mwingine, alifiwa na mume wake wa kwanza akiwa na miaka mingapi. Huenda hapo alipo amekaa kwenye ujane miaka 15, kwanini asitoe machozi ya furaha mbele za Mungu.
Watu wanaweza kuona kwanini unamshukuru Mungu kwa machozi mengi kwa kujenga tu nyumba, wakati ni kitu cha kawaida tu. Huwezi kujua mtu yule ametumia nguvu kiasi gani, huwezi kujua msoto aliopitia kuikamilisha hiyo nyumba.
Huwezi kuelewa sana kwanini mtu anatoa shukrani huku akidondosha machozi kwa kusafiri na kufika salama, huwezi kujua yaliyompata katikati ya safari yake.
Wengi tunaona kutoa machozi ni jambo la watu wasiostarabika, wengi tunaona kutoa machozi ni suala wa watu fulani wenye dhiki sana. Inafika kipindi mtu anakuwa mkavu kiasi kwamba unaona kabisa huyu mtu ni wa mwilini sana.
Sikufundishi kuwa mtu wa kulialia ovyo bila mpangalio, yapo mambo yanayogusa maisha yetu, yapo mambo aliyotutendea Mungu. Kiasi kwamba hatuwezi kujizuia kutoa machozi yetu, japo upo wakati pia wa kumlilia Mungu, ila haya yanakuwa machozi kwa ajili ya kufanikisha au kutendewa jambo fulani zuri.
Haya tunajifunza zaidi hapa;
Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha; hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikilikana mbali sana. EZR. 3:12-13 SUV.
Umeona hapo👆🏽👆🏽 wakapiga kelele za furaha baada ya kukamilika nyumba ya Mungu wao, mpaka watu wengine wakashindwa kutofautisha kelele za furaha au za huzuni.
Kwanini ujizuie furaha yako mbele za Mungu, kwanini watu wanakunyima uhuru wa kujiachia mbele za Mungu wako. Wakati una jambo ambalo Mungu amekutendea, na kwa akili za kibinadamu lilishindikana kabisa.
Kuanzia leo uwe huru mbele za Mungu kwa kile Mungu amekutendea, kuwa huru mbele za Mungu sio kuvunja taratibu za kanisa zilizowekwa, ni kwa sababu umeijua kweli kupitia Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.