Mungu kukupa jukumu la kuitenda kazi yake, alishakuandaa kwa ajili ya kazi hiyo kabla ya kuzaliwa kwako. Unapoanza kutoa sababu za kukataa wito wako, utakuwa unaangalia sana mwilini kuliko rohoni.
Hili linawakumbuka wengi sana hasa vijana, wanaposikia kuitwa kwao, huwa wanatengeneza sababu nyingi za kukataa huo wito wa Mungu. Kukataa kwao hakuwezi kuondoa lile kusudi la Mungu aliloweka ndani yao.
Tunaweza kuwa tumezoea kumwona mtu anapoanza utumishi, lazima awe na umri fulani mkubwa. Inapotokea kinyume na hapo, tunaanza kutilia shaka ya yule mtu aliye na umri tofauti na tuliozoea.
Tamaduni zetu zinaweza kutuaminisha vitu fulani ambavyo hupelekea kufikiri tupo sawa kwa kila kitu. Bila kuangalia maandiko matakatifu yanasemaje, tunaweza kuamini zaidi miiko ya tamaduni zetu, bila kujua tunategeneza uoga kwa mambo ya Mungu.
Hili jambo lilimkumba nabii Yeremia, wakati Mungu anamkusudia aanze kumtumikia, alianza kukwepa jukumu hilo kwa kutoa sababu ya kuwa yeye ni mtoto. Yeremea sio kwamba alikuwa mtoto kama tunavyojua mtoto, labda ni vile hakuona/hakuwahi kuona nabii wa umri wake.
Rejea: Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, SIWEZI KUSEMA; maana mimi ni MTOTO. Lakini BWANA akaniambia, USISEME, MIMI NI MTOTO; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. YER. 1:6-7 SUV.
Mungu anamhakikishia Yeremia atakuwa pamoja naye, na kila mahali atakapomtuma, alipaswa aende. Maana Mungu alikuwa pamoja naye kila hatua za utumishi wake.
Tena Mungu anamhakikishia Yeremia atamwedhesha kusema mbele za watu, ambapo hili pia ni tatizo la wengi. Huwa wanafikiri sana wataanzaje kuhubiri mbele za watu, hili jambo la kuongea tunaliona pia tunaposoma habari ya Musa wakati Mungu anamtuma.
Usiogope ndilo Neno lake Mungu, alilomwambia nabii wake Yeremia, alimhakikishia kabisa hofu aliyonayo, aiondoe kabisa ndani yake.
Rejea: Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA. Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kungoa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. YER. 1:8-10 SUV.
Huenda hapo ulipo, umeshiriki kukatisha tamaa vijana wanapoinuka kwa utumishi wa Mungu. Umejaribu kuleta uzoefu wako wa kibinadamu, bila kutazama kusudi la Mungu huwa halizuiliwi na umri wa mtu.
Huenda hapo ulipo, ulijiona mdogo, umefika mahali ukasema ngoja ukue kwanza. Umeshangaa baada ya kusema hivyo, hujawahi kupata amani ndani ya moyo wako, kila siku unasikia nenda katagaze ukuu wa Mungu.
Unapaswa kuinuka uende, Mungu anakutaka umtumikie yeye, maneno ya wanadamu yasikusumbue, aliyekuita anafahamu hayo yote. Anajua unaweza, maana alishakuandaa tangu ukiwa tumboni mwa mama yako.
Kusingizia una umri mdogo, unasubiria hadi ukue kue kwanza, huko ni kutafuta namna ya kukwepa majukumu yako. Mungu haangalii kama mwanadamu aangaliavyo, Mungu kuweka wito ndani yako, jua ameshakuandaa na atakuongoza yeye mwenyewe.
Haijalishi upo kwenye mazingira gani magumu, ukimruhusu Mungu kwa kukubali kile anataka ukifanye. Uwe na uhakika atakuwa na wewe siku zote za utumishi wako, utakaokuwa nao hapa Duniani.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081