Baruku alikuwa ni mwandishi mzuri sana wa vitabu aliyekuwa anaandika jumbe mbalimbali kutoka kwa Mungu. Pale nabii Yeremia aliposema na Mungu wake, aliyekuwa anaandika jumbe zile alikuwa ni Baruku.

Baruku alitumika katika eneo hilo la uandishi wake wa vitabu, na kazi yake Mungu aliitambua sana. Kama ilivyo leo kila mmoja Mungu anamtambua katika eneo lake la utumishi mwema.

Huyu Baruku mwandishi wa vitabu vilivyotoka kwenye kinywa cha nabii Yeremia, alifika mahali akachoka kwa kuugua kwake. Akawa haoni raha yeyote kama wengine.

Mungu akatuma ujumbe kupitia nabii wake Yeremia, kumweleza kwamba, tazama, yote yaliyojengwa yatabomolewa, na yote yaliyopandwa yatang’olewa. Lakini yeye Baruku roho yake itakuwa salama na atapata ulinzi wa Mungu mahali pote atakapokwenda.

Rejea: Basi, mwambie hivi, BWANA asema hivi, Tazama, niliyoyajenga nitayabomoa, na niliyoyapanda nitayangoa; na haya yatakuwa katika nchi yote. Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema BWANA; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda. YER. 45:4‭-‬5 SUV.

Habari hii inatufunza nini, yapo mengi yakujifunza ila napenda kukushirikisha machache. Ili uweze kuona ulipo Mungu hajakuacha hata kama unapita magumu.

Huenda umejitoa sana kwenye mambo ya huduma ya Mungu, maisha yako yote umekuwa mtu wa kumtumikia Mungu.

Pamoja na kutumika sana, kuna hatua umeitamani siku nyingi kama mwanadamu ila hukufanikiwa kuifikia. Zaidi sana, ulizidi kuona wengine wakifanikiwa katika maisha yao ya kimwili ila wewe hukupata mafanikio hayo.

Umefika mahali umekuwa mtu wa kuugua tu, huna furaha na maisha yako. Kila siku umekuwa mtu wa kwenda hospital, ukinywa dawa hii, wiki hii, wiki ijayo unabadilishiwa dawa nyingine.

Imefika hatua hata wale ndugu zako, watumishi wenzako, marafiki wenzako, na wafanyakazi wenzako. Wanakuona kama vile umemkosea Mungu wako, yale unayopitia wanaona kama ni pigo/laana ya Mungu kwako.

Mungu anamwambia Baruku, hayo yote unayoyaona na kuyatamani, usiyatamani, maana nitayaharibu yote. Lakini wewe utakuwa salama.

Rejea: Basi, mwambie hivi, BWANA asema hivi, Tazama, niliyoyajenga nitayabomoa, na niliyoyapanda nitayangoa; na haya yatakuwa katika nchi yote. Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema BWANA; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda. YER. 45:4‭-‬5 SUV.

Kama mwanadamu huenda hapo ulipo umetamani siku nyingi kuwa na nyumba nzuri, na katika utumishi wako wote ulikuwa hujafanikiwa kuwa na hiyo nyumba. Mungu ana kusudi jema nawe, hata hizo nyumba unazozitamani zinaenda kuharibiwa zote.

Huenda hapo ulipo umeokoka na umekuwa mwaminifu mbele za Mungu, umekuwa ukitafuta upate kazi nzuri. Hiyo kazi unayoitamani, inaenda kusambaratika yote, na Mungu kukuinulia kazi nyingine nzuri.

Huenda hapo ulipo wenzako ofisini wamekuwa wakija siku chache na kupata nafasi za juu ila wewe upo hapo mwaka wa kumi sasa. Hakuna kupandishwa cheo chochote, Mungu anasema hata hiyo nafasi unayoitamani, inaenda kufa.

Mtazame Mungu wako, tumaini lako liwe kwa Mungu, usiache imani yako kwa kuona Mungu amechelewa kujibu maombi yako. Sio kwamba unaomba vibaya, sio kwamba unatenda dhambi, Mungu analo kusudi jema kwako.

Huenda ndoa yako imekuwa ikikuhuzunisha kila siku, pamoja na kumtumikia sana Mungu, hajaweza kumbadilisha mke/mume wako. Umeomba sana kuhusu mume/mke wako, lakini hakuna badiliko lolote uliloliona kwake, Mungu yupo anaenda kusambaratisha yote mume/mke wako anayojivuna nayo.

Huenda mume/mke wako anakusumbua sana, kwa sababu ya kazi yake, kwa sababu ya cheo chake ofisini/serikalini. Mungu anasema vyote anaenda kuvibomoa na kuving’oa, hakuna kitu atabaki nacho.

Bila shaka kuna hatua umevuka baada ya kusoma ujumbe huu, elewa hakuna hasara kumtegemea Mungu, na hakuna hasara kumtumikia Mungu. Daka hili litakusaidia katika utumishi wako, haijalishi eneo unalomtumikia Mungu hakuna analoliona. Fahamu Mungu analiona, na ipo siku utavuna matunda ya utumishi wako.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.