Mazingira magumu sawa, pana njaa sawa, hakuna huduma muhimu sawa, pana mauaji sawa, na pana uharibifu wa mali zako sawa.

Kazini kwako pana manyanyaso sawa, nyumbani kwenu kila siku masimango sawa, kwa ndugu yako unayeishi naye anakutesa sawa, na shuleni kwenu unanyanyaswa sawa.

Umefika mahali unatamani kukimbilia mahali pengine ukapumzike, kama ni kazi nzuri unaweza kupata sehemu nyingine, kama ni kelele za wazazi unao uwezo wa kuondoka nyumbani.

Pamoja na hayo yote, unapaswa kumsikiliza Mungu anasemaje kuhusu hali yako. Kama Mungu anakutaka ubakie hapo hapo kwenye hali ngumu unayopitia sasa, unapaswa kumtii Mungu wako.

Kuna wakati nikawa naongea na dada yangu mmoja, akawa ananiambia mimi naacha kazi, naomba uniombee barua yangu ya kusitisha mkataba ikubaliwe.

Binafsi sikupokea vizuri taarifa zile, ilibidi nimjibu vile najisikia moyoni mwangu, nilimwambia siwezi kuomba maombi ya wewe kuacha kazi. Maana napenda kukuona ukiwa Kwenye hiyo kazi, tena Mungu amekuweka hapo kwa kusudi lake.

Kama kazi uliomba sana Mungu akupe, sasa amekupa hiyo nafasi, kuanza kutaka kuondoka, inakuwa ni jambo lingine.

Huyu ndugu mazingira ya kazi yalimfanya aichukie kazi yake ghafla, lakini kuwepo Kwenye kazi ile haikuwa bahati mbaya. Lipo kusudi maalum kabisa la yeye kuwa mahali pale.

Wakati mwingine tunapokutana na changamoto ngumu katika mazingira ya kazi, hatupaswi kutafuta kukimbia. Pale pale kwenye ugumu Mungu ndio anapanga kutubarikia humo humo, na hataki tukimbilie mahali pengine.

Hili tunajifunza kwa watu wa Yuda waliobaki kidogo baada ya wenzao kuawawa wote. Mungu anawaambia wasiondoke, wala wasikimbilie Misri mahali ambapo hakuna njaa.

Rejea: Ikawa, baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia. Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi; Ikiwa mtakaa bado katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawangoa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda. YER. 42:7‭-‬10 SUV.

Wanaambiwa wasihame, haijalishi uchache wao, haijalishi walipo kuna njaa, haijalishi mfalme ni tishio kwao. Mungu anawaambia wabaki pale pale.

Sijui wewe unataka kukimbia nini katika maisha yako, Mungu anakwambia siku ya leo, baki hapo hapo atakubarikia mahali ulipo. Ukikimbilia mahali unapopaona pazuri kwako alafu Mungu hajakuruhusu uende, utaenda kukutana na shida zaidi ya hiyo.

Rejea: Lakini mkisema, Hatutaki kukaa katika nchi hii; msiitii sauti ya BWANA, Mungu wenu; mkisema, La! Lakini tutakwenda nchi ya Misri, ambayo hatutaona vita, wala kuisikia sauti ya tarumbeta, wala kuona njaa kwa kukosa chakula; nasi tutakaa huko; basi, lisikieni neno la BWANA, enyi mabaki ya Yuda; BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ikiwa mwakaza nyuso zenu kuingia Misri, na kwenda kukaa huko; basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko. Haya ndiyo yatakayowapata watu wote waelekezao nyuso zao kwenda Misri, na kukaa huko; watakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesalia, au kuokoka katika mabaya nitakayoyaleta juu yao. YER. 42:13‭-‬17 SUV.

Inaweza kuwa njaa ni kali sana, unatamani kuwakimbia watoto wako, usifanye hivyo, Mungu atakupa njia ya kupona na njaa hiyo.

Inaweza kuwa mume wako amekuwa kikwazo kwako, umefika mahali unataka kuachana naye kwa siri. Tulia Mungu anaenda kumbadilisha tabia yake mbaya, endelea kumwombea.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081