Ukiwa sio mvivu, huwezi kukosa kazi ya kufanya katika maisha yako, kazi zipo nyingi sana za kufanya. Inategemeana na wewe ni namna gani unachagua kazi ya kufanya.

Ukikosa kitu cha kufanya watakuja watu watakupa kitu cha kufanya, inabaki kazi kwako sasa utakifanya vizuri hicho ulichopewa au utakifanya kawaida, au utakifanya vibaya au kizembe.

Sasa wengi wetu huwa tunafanya vibaya au tunakuwa sio wavumilivu katika kazi tunazopewa na waajiri wetu. Tunafanya kidogo na kuanza kutaka tupate matunda ya haraka kwa kazi ya muda mfupi.

Bila kujua tunahitaji kuweka bidii kubwa katika kazi, siku zote unapaswa kuelewa hili. Kazi yeyote utakayopewa inahitaji uweke kazi haswa ili aliyekupa hiyo kazi aendelee kukulipa zaidi.

Kama ni kazi ya siku moja, wengi huwa tunafanya kazi hizo kizembe mpaka inapelekea yule aliyetupa hiyo kazi. Asiweze kutupa tena na kesho, hii hupelekea kuwapa watu wengine wenye uwezo wa kuifanya hiyo kazi.

Laiti tungekubali kuwa watu wa kazi, leo hii usingemkuta kijana amekaa bila kazi yeyote ya kufanya. Vijana wengi au watu wengi wanashinda kutwa nzima bila kufanya kazi kwa sababu ya uvivu na kuchagua kazi.

Uvivu upo ndani yetu ila tunapaswa kuukataa kwa nguvu zetu zote, tunapoukataa uvivu tunapaswa kuelekeza nguvu hizo kwenye kazi.

Ukiwa kama mtu aliyeokoka, unapaswa kuwa mtu wa kazi, ukiwa kazini fanya kazi kweli kweli, ukiwa huna kazi alafu ukapewa kazi. Hakikisha unaifanya kazi hiyo vizuri ili siku nyingine watu wasikukwepe na kuwapa watu wengine.

Msemo wa sina ajira hujaanza kuzungumzwa leo, wala malalamiko ya ajira hayajaanza leo. Tangu zamani zile hili jambo lilikuwepo, lakini kulikuwepo kazi za kufanya hata kama zilikuwa za siku moja.

Rejea: Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu. MT. 20:6‭-‬7 SUV.

Umeona hapo, hawa watu walikutwa wamesimama mchana kutwa bila kazi. Lakini walivyopewa kazi ya kwenda shamba la mizabibu hawakukataa, wala hawakusema hiyo kazi ya shamba sisi hatuendi.

Ndugu kama unaona haya kufanya kazi ndogo ndogo za kuweza kukuingizia pesa, kwa sababu ya elimu yako kubwa. Nikueleze ukweli utaendelea kulalamikia serikali haikupi ajira.

Usichague kazi, fanya kazi yeyote ilimradi ni halali, usiangalie elimu yako, usiangalie watu watakuonaje ukiwa kwenye hiyo kazi. Wewe piga kazi na Mungu atakuinua kwenye hiyo hiyo kazi inayoonekana ni ya kawaida.

Baada ya kazi utalipwa, lakini ukiwa umekaa tu bila kufanya kazi huku ukilalamika. Hakuna atakayekulipa kwa malalamiko yako, utalipwa kwa kazi, elewa hili siku zote.

Rejea: Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. MT. 20:8 SUV.

Biblia ipo wazi kabisa kuhusu hili ninalokueleza hapa, unaona hapo? Kila mmoja alipwe ujira wake. Sasa kama hawakufanya kazi wangelipwa? La hasha wasingeweza kulipwa.

Fanya kazi ili ulipwe, fanya kazi ili upate fedha.

Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com