Kujiona tunajua sana kupenda kuliko watu wengine, imetugharimu maeneo mengi sana katika maisha yetu ya ndoa.
Mtu anaona kila dalili za mdada/mkaka anayetarajia kuanza naye maisha ya ndoa siku chache zijazo. Anamhangaisha kila siku, Mungu amejaribu kumwonyesha jinsi alivyo na tabia mbaya. Bado utakuta mtu ameng’ang’ana tu na huyo dada/ kaka.
Anachosimamia yeye, ni kwamba anaona hawezi kupata mwanaume/mwanamke mwingine zaidi ya huyo. Anaona bora alazimishe kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye tayari Mungu alishamtahadharisha kabisa kuwa sio mtu sahihi na salama kwake.
Mungu kutukataza kuingia kwenye mahusiano ya ndoa na mtu tunayemwona sisi anatufaa, wakati mwingine sio kwamba ni mtu mwenye tabia mbaya. Anatuzuia kuingia naye kwenye ndoa, kwa sababu hana muda mrefu atakufa.
Unapoingia naye kwenye ndoa, uwe na uhakika utabaki mjane, na uwe na uhakika utabaki mgane. Wakati ulikuwa na uwezo kuepuka hayo mapema, kufiwa na mume ukiwa binti mdogo, itakupa shida sana kuolewa haraka.
Mungu anapokuzuia usioe/usiolewe na jamii fulani, usiwe mkaidi, Mungu anajua zaidi yako, Mungu anaona kesho yako. Utapokaidi maelekezo yake, kwanza utakuwa umetenda dhambi, na utakuwa umejiingiza kwenye majonzi ambayo hayakustahili kabisa uyapate.
Wakati mwingine unaweza kushawishiwa na watu uzae tu na mtu wa jamii ile, usiondoke mahali pale bila kuacha alama. Unajazwa maneno mengi, maneno yenye uasi ndani yake, ukaona ni kweli ngoja utembee na mdada/mkaka mmoja wapo. Bila kujua huyo uliyezaa naye, na huyo mtoto uliyemzaa, hawatachukua muda mrefu watakufa.
Wakati mwingine Mungu anamzuia mtu asiolewe/asioe, kwa sababu mwanamke unayetaka kumwoa, na mwanaume anayetaka kukuoa. Hamtakaa naye muda mrefu, atakuletea ugonjwa wa ukimwi kwenye ndoa yako.
Hili tunajifunza kwa nabii Yeremia, aliambiwa na Mungu asioe, kwa sababu Mungu alipanga kuangamiza watu mahali pale.
Rejea: Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa. Maana BWANA asema hivi, katika habari za wana, na katika habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na katika habari za mama zao waliowazaa, na katika habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii; watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi. YER. 16:1-4 SUV.
Hebu fikiri umeoa/umeolewa mahali kama hapa alivyokatazwa nabii Yeremia, unafikiri ndoa yako itakaa muda mrefu? La hasha haitachukua muda mrefu, utaona jambo baya likitokea kwenye ndoa yako, ambalo linaweza kukuathiri na wewe. Maana tayari umeshajiungamanisha na undugu wa mahali pale.
Muhimu sana kuwa makini, hasa kwa wale ambao bado hawajaolewa/ hawajaoa, itawasaidia sana kuepukana na mambo ambayo wangemsikiliza Mungu yasingewakuta.
Usikimbilie kusema muda umeenda sana ukiwa hujaoa/hujaolewa, ukajidumbukiza kwenye mahusiano yeyote. Gharama yake ni kubwa kuliko kuchelewa kuoa/kuolewa, bora ukachelewa kuoa/kuolewa, ukaja kuoa/kuoelewa na mtu sahihi aliyekusudiwa na Mungu wako.
Narudia tena, kuwa makini mno kwenye eneo hili la mahusiano, msikilize Mungu wako kuliko vyote. Usiendeshwe sana na tamaa za mwili, ukajitupia kwenye mahusiano mabovu ya ndoa, utajuta kuzaliwa.
Nimekupitisha kwenye hayo maandiko matakatifu uweze kuona hili jambo lilivyo na uzito wake, ukijua ndoa ni maisha, na sio kitu cha kufanya haraka haraka. Utakuwa makini sana kwenye eneo hili, umakini ambao utakusukuma uwe unamwomba sana Mungu akukutanishe na mwenzi wako sahihi wa maisha.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.