Miaka ya nyuma kidogo wakati naanza kusoma soma vitabu mbalimbali vikiwepo vya watumishi wa Mungu, nilikutana na kitabu kimoja cha MAISHA YANAYOONGOZWA NA MALENGO kilichoandikwa na Rick Warren. Ni kitabu kizuri sana nilijifunza mengi sana ndani yake.

Moja ya mambo niliyojifunza ilikuwa namna ya kuweza kusuluhisha watu waliokosana, moja ya kitu nilichojifunza na mpaka leo kimekaa moyoni na ninakitumia sana maeneo mengi. Ni kutopendelea upande wowote unapogundua umekosea, haijalishi ni marafiki, ndugu, au wazazi wako. Unapaswa kusema wewe ulikosea hapa na pale.

Nimejisikia furaha sana mara nyingi pale ninapojikuta nipo katikati ya watu wanaolaumiana na kumwona mwenzake ana makosa. Lakini ukisikiliza chanzo chake mpaka kufika hapo walipofikia, unaona kabisa lipo tatizo lilianzia kwa huyohuyo anayejiona hana kosa.

Shida ya wasuluhishi wengi wa migogoro, huwa wanafeli kwa kumwogopa kumwambia mtu ukweli kwa kosa lake. Badala yake wamekuwa wakikandamiza upande mmoja, ili kulinda mahusiano ya upande wa mkosaji usije ukaharibika.

Vizuri ukajifunza hili ili usiwe unavutwa na upande mmoja kukandamiza upande mwingine pale unapojikuta unasuluhisha mgogoro wowote ule. Utakapoona lipo tatizo kwa mmoja wapo, kuwa mkweli kwa kuwaweka wazi wote.

Ukweli siku zote huwa huwezi kuuchanganya na uongo, Lazima utafika hatua ukweli utajitenga na uongo nao utajitenga kivyake. Mtu akimkosea mwenzake usiogope kumweleza kwa sababu ni rafiki yako wa Karibu sana, badala yake ukamua kuelekeza shutuma kwa mwenzake asiyehusika.

Ili uwe msuluhishi mzuri wa ugomvi wowote, usiangalie ukaribu wako na moja kati ya hao unaotaka kuwasuluhisha. Usiangalie upande unaojuana nao ukauacha alafu ukaukandamiza ule usiofahamiana nao ukautupia lawama za makosa.

Maandiko Matakatifu yanaliweka wazi na kulithibitisha kwa uwazi hili jambo;
Tafadhali, nisiupendelee uso wa mtu; Wala sitajipendekeza kwa mtu ye yote. AYUBU 32:21 SUV.

Hebu jiulize umejipendekeza kwa wakubwa wangapi kutetea ujinga, hebu jiulize umetetea mangapi maovu kwa kumwogopa mtu mmoja ukawatupia mzigo wa lawama wasiohusika?

Umeamua kuwa msuluhishi chunga sana kitu kinaitwa upendeleo wa kuegemea upande mmoja ambao una mahusiano nao ya karibu. Kama ni mke/mume wako ukakutana na ugomvi na mtu mwingine mwambie hapa ulikosea kama ataonekana na kosa, hata awe ni mzazi/mlezi wako ukimkuta amemkosea mtu mwingine na ukapata nafasi ya kusikiliza malalamiko ya pande zote mbili mweleze hapa ulikosea.

Haya yote unanena si kwa mashindano, bali kwa hekima na kutaka kujenga palipobomoka. Ili kila mmoja aondoke akiwa huru ndani ya moyo wake, isitokee aliyekosea akaonekana hana kosa, na asiyekosea akaonekana ana kosa.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.