Mke na mume

“Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako”, Mal 2:14 SUV.

Wanaume wengi wa Kiyahudi baada ya kutoka uhamishoni walikuwa siyo waaminifu kwa wake zao ambao waliwaoa katika ujana wao.

Walikuwa wanatafuta sababu kuwapa talaka(kuwaacha), kwa sababu walitaka kuoa wanawake wengine waliowataka wao.

Bwana alichukizwa sana na tabia hii ya ubinafsi, akisema kwamba amewafanya mume na mke kuwa mmoja(yaani mwili mmoja).

“Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana”, Mal 2:15 SUV.

Kwa sababu ya dhambi hii Mungu amewageuzia kisogo wenye dhambi na kukataa kusikia maombi yao.

“Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya BWANA kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia. Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako”, Mal 2:13‭-‬14 SUV.

Siku za leo hili sio jambo geni, wanaume baadhi huacha wake zao kwa tamaa zao wenyewe, hasa wale wake walioanza nao maisha.

Wanapofanikiwa huona hao wanawake hawana hadhi ya kuwa nao, wanaamua kuwaacha na kutawafuta wanawake wengine.

Jambo hili linavuruga familia na kuleta shida kwa wale watoto waliozaliwa, hata mwanamke anakuwa ameingia kwenye shida.

Tukiacha kuwa jambo hili ni chukizo mbele za Mungu, kuachana kunavuruga mambo mengi sana, fikiri mwanamke aliyekaa kwenye ndoa miaka 10 alafu anaachwa.

Mwanamke huyu anaweza kubaki hivyo bila kuolewa, kisa tu aliachwa na mwanaume mmoja mwenye tamaa za mwili.

Wanaume tusiwe na hii tabia, Mungu hapendezwi kabisa na kuachana, tamaa mbaya isikupelekee ukamwacha mke wa ujana wako.

Mungu atusaidie sana
Soma neno ukue kiroho
Samson Ernest
+255759808081