
Katika maisha yetu ya kila siku tumejikuta tukiwa na watu wanaotusaidia kazi zetu, anaweza akawa mfanyakazi wa ndani, anaweza akawa kwenye kampuni yako, anaweza akawa kwenye duka lako.
Anaweza akawa mtu anayechunga ng’ombe zako, anaweza akawa ni mtu anayelima mashamba yako, anaweza akawa dereva wako.
Watu hawa wanaotusaidia kazi wanafika mahali wanakuwa ndugu kabisa, kutokana na kuishi nao karibu kwa muda mrefu.
Watu hawa wanaotusaidia kazi sio miaka yote tutaendelea kuishi nao, wapo itafika mahali watapenda kuendelea na maisha yao mengine.
Watu kama hawa waliotusaidia kazi kwa miaka mingi, hatupaswi kuwaacha hivi hivi mikono mitupu. Tunapaswa kuachia kitu cha kuwasaidia watapokuwa hawapo pamoja na sisi.
Nimeona baadhi ya watu au familia wakifanya hivyo, unakuta mtu alikuwa mfanyakazi wa ndani anasomeshwa hadi anamaliza shule/chuo.
Nimeona wengine wakiwa wanauziwa maduka yao ila mwisho wa siku anamfungulia duka lake huyo aliyekuwa anamuuzia duka lake.
Hiyo ni mifano michache, yapo mambo mengi mazuri waliyofanyiwa wafanyakazi, na mambo haya ni mambo yanayompendeza Mungu sana.
Wanaofanya hivi wanafanya vitu vya kiMungu kabisa, na Mungu anapenda watu wa namna hiyo. Kufanya hivyo ni kuonyesha shukrani kwa mtu aliyetoa maisha yake kumtumikia.
Mungu aliwapa maelekezo haya wana wa Israel kipindi cha Musa, vile ambavyo wanapaswa kuwatendea watumwa wao.
Rejea: Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako. Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu; umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia BWANA, Mungu wako. KUM. 15:12-14 SUV.
Leo sio wana wa Israel, isitoshe utaratibu wa kuwa na watu wa kutusaidia kazi bado unaendelea katika maisha yetu ya kila siku.
Sisi tuliokoka tunapaswa kujua hili na kulitendea kazi, ili wale wanaopita kwenye mikono yetu wamtukuze Mungu kupitia sisi.
Tena tutakuwa tumewasaidia wengi sana walio nyuma ya huyo tuliyemtendea jambo jema la kumsaidia katika maisha yake.
Usipende sana kukaa na watoto wa watu alafu wanakuja kuondoka mikono mitupu, utakuwa umefanya jambo lisilo jema kabisa.
Mtu aliyefanya kazi kwako kwa bidii, kwa moyo wake wote, kwa uadilifu, haijalishi alikuwa anafanya kazi gani. Maadam amekaa na wewe muda wa kutosha na amekutumikia vizuri, usimwache aondoke mikono mitupu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com