Wapo watu wanasema wao ni watumishi wa Mungu, Mungu amewatuma, lakini ukiangalia utendaji wao wa kazi ya Mungu, unaona kabisa wanachosema na wanachotenda ni vitu viwili tofauti kabisa.

Kinachomtambulisha mtu kuwa ni mtumishi wa Mungu, au sio mtumishi wa Mungu ni ule utendaji wake wa kazi ya Mungu. Kazi yake ndio inamtambulisha yeye ni mtu wa namna gani, kama ni mtumishi wa Mungu kweli atajulikana kupitia kazi zake, na kama sio mtumishi wa Mungu napo atajulikana kupitia kazi zake.

Utumishi wetu mbele za Mungu, ndio kitambulisho chetu mbele za watu, hatuhitaji kutumia nguvu kubwa sana ya kuwaaminisha watu wengine kuwa sisi ni watumishi wa Mungu aliye hai.

Kazi zetu ndio zinatufanya tutambuliwe na watu kuwa ni watumishi wa Mungu, tunamhubiri Yesu Kristo sawasawa au tunafanya yaliyo kinyume na maagizo yake.

Kazi za mtumishi wa Mungu wa kweli, zinamhubiri Yesu Kristo kwa uwazi na wale wanaosikia wanachagua wenyewe wawe watoto wa Mungu au wabaki na maisha yao ya upotofu.

Mtu anayezitenda kazi za Mungu, atamdhihirisha Yesu Kristo katika mafundisho/mahubiri yake kwa uwazi kabisa, hatakuwa na kona kona za kupotosha watu kuhusu kweli ya Mungu.

Mtu anayezitenda kazi za Mungu, kila jambo zuri atakalolifanya atamwacha Yesu Kristo ajitwalie utukufu wake. Maana anajua si kwa uwezo wake ayatendayo hayo, bali ni kwa uweza wa Yesu Kristo uliokuwa ndani yake.

Tofauti kabisa na mwalimu, mchungaji, mwinjilisti, mtume, na nabii, anayefanya kazi ya Mungu kwa kutafuta sifa zake mwenyewe, ama kwa kutafuta kutukuzwa yeye mwenyewe. Huyu atakuwa sio mtumishi wa Mungu hata kama yeye anasema anazitenda kazi za Mungu.

Yesu Kristo mwenyewe aliliweka wazi hili jambo, wale waliokuwa na mashaka naye, aliwaambia kama hazitendi kazi za Baba yake aliye juu mbinguni, wasimwamini kabisa ila kama anazitenda kazi za Mungu, waziamini hizo kazi. Je, kwetu sisi si zaidi ya hapo? Lazima kazi zetu zimdhihirishe Mungu wetu.

Rejea: Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba. YN. 10:37‭-‬38 SUV.

Huenda ulikuwa unapata tabu kuhusu hili, na kujiuliza ni nani mtumishi wa Mungu wa kweli, na nani si mtumishi wa Mungu wa kweli. Fahamu kwamba mtumishi wa Mungu anatambulishwa na utendaji wake wa kazi ya Mungu.

Unaweza usimwelewe sana mtu kutokana na alivyokaa, kupitia kazi zake, zinazomdhihirisha Yesu Kristo, inaweza ikawa njia nzuri ya kumtambua mtu huyo.

Maneno matupu hayatasaidia kitu, kazi za Mungu anazozifanya mtu wa Mungu, ndio zinaweza kumsemea kwa watu kuwa yeye ni nani. Walio na Roho wa Mungu ndani yao hawatakuwa na mashaka naye tena.

Kama Yesu Kristo yupo ndani yako, na wewe upo ndani yake, zifanye kazi zake, hata kama watu watatokea wasikuamini haraka, watakapozitazama kazi zako zilizomwinua Kristo maeneo mbalimbali katika maisha ya watu. Watu hao lazima waziamini hizo kazi, na watakapoziamini hizo kazi, watakuamini na wewe.

Sitaacha kukuambia usome Neno la Mungu, kama unapenda kukua kiroho na kumtumikia Mungu vizuri, hakikisha unakuwa na muda wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu. Karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group uungane na wenzako wanaosoma Neno kila siku, wasiliana nasi, +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com