Kuanza kujuta kwenye ndoa huwa inaanza mapema sana kabla humjaanza kuishi pamoja kama mume na mke, japo wakati bado hamjaoana huwa sio rahisi sana kujua hilo.
Kuna watu wanahangaishwa sana na sura kuliko tabia nzuri ya mtu, kuna watu wanaona sifa na wanajisikia fahari sana kuwa na mwanamke mwenye sura nzuri ni jambo nzuri sana na la msingi. Lakini huyo mwenye sura nzuri anaweza akawa na tabia fulani mbaya ambazo haziendani kabisa na uzuri wake wa nje.
Ndani ya Biblia wapo watu wametajwa wenye sura nzuri na wapo watu sasa wana sura nzuri kweli, hili halina ubishi, changamoto inakuja pale tunapoangalia sura zaidi na tukasahau ule uzuri wa ndani ambao unahitaji upige goti mbele za Mungu.
Unapoingia kwenye mahusiano ya ndoa na mtu ambaye anakuona mbaya wa sura ila kuna vitu ambavyo vimemsukuma akuoe/umwoe. Labda kwa sababu alikuwa na hamu ya kuoa/kuolewa, Labda kwa sababu anayemwoa au anayeolewa naye ana uwezo wa kifedha. Huyo mke/mume wa kigezo hicho atakusumbua tu.
Mwanamke ukiolewa na mwanaume ambaye anakuona mbaya wa sura, labda alikuoa kwa msukumo wa ndugu zake au wewe mwenyewe ulijilazimisha kuolewa naye. Uwe na uhakika utafika mahali utaanza kujuta kwa nini uliolewa na huyo mwanaume, maana utakuwa unaona dhaharau zake waziwazi kwako.
Mwanaume ukioa mwanamke ambaye tayari alishakuona wewe si wa viwango vyake ila amekubali kuolewa na wewe kwa sababu ya uwezo wako kifedha. Mwanamke huyo atakusumbua sana na kama hana hofu ya Mungu, hataona aibu kumtafuta mwanaume mwingine anayemwona yeye ni mzuri, atembee naye.
Ndio maana ni muhimu sana kuweka pembeni matamanio ya nje, ndio maana ni muhimu sana kumwomba Mungu akukutanishe na mume/mke wako. Ukitumia tu akili zako za kibinadamu bila kumshirikisha Mungu, huwezi kujua huyo aliyekubali uingie naye kwenye ndoa amependea nini kwako.
Nazungumza na mtu ambaye bado hajaoa/hajaolewa, usije ukaingia kwenye ndoa na mtu ambaye unamwona moyoni mwako huna amani naye kutokana na sura yake ilivyo mbaya kwako. Hakuna mtu aliyekamilika hata ukimtafuta hutampata, ndio maana wewe mwenyewe una mapungufu yako.
Linapokuja suala la ndoa, sio suala la kuchukulia kawaida, hakuna kitu kinaumiza moyo kama kusikia mke/mume wako anakuambia mtu mwenyewe sura mbaya. Limeolewa na wewe kwa basi tu au nimekuoa kwa basi tu.
Huyo unayemewona mbaya kwako, yupo atakayemfaa, huyo unayemewona mzuri, yupo ambaye hamfai, ndio maana kwenye size za viatu. Kuna mtu anavaa namba 8, na mwingine anavaa namba 9, na sio kila kiatu chenye size ya mtu anayevaa hicho kiatu atakipenda.
Kama vile mambo yanakuwa magumu sio! Baada ya kukueleza haya? Hapana mambo siyo magumu, cha msingi hapa ni kuwa mtulivu katika eneo hili. Usije ukavutwa sana na sura nzuri ambayo kila mtu akimtazama anasema hakika Mungu aliumba watu wazuri. Alafu ukasahau kuangalia tabia, ukasahau kujua uliyempenda ni wa kufanana na wewe kweli?
Unaweza kusema nikishamwoa/nikishaolewa naye nitampenda huko huko kwenye ndoa, kama imeshindikana kumkubali mkiwa wachumba, kwenye ndoa hakuna kitakachobadilika sana. Msingi mzuri wa ndoa yako upo kwenye uchumba, ni kipindi ambacho unajipima utaweza kuishi na huyo mwanaume/mwanamke maisha yako yote? Na kipindi cha kujua uliongozwa na tamaa zako katika kuchagua au Mungu mwenyewe amewakutanisha pamoja.
Ni kama kitu hakina maana sana “sura tu au uzuri tu” unaweza kufikiri hivyo ila kama utakuwa na mke anayekupenda kweli alafu humpendi sura yake, kutakuwa na shida. Na kama utakuwa na mume ambaye yeye anakupenda kweli ila wewe sura yake inakupa shida na kukukosesha amani ya moyo, hiyo ndoa itakuwa mzigo kwako.
Chagua kitu roho inapenda na uwe na uhakika na chenyewe kinakukubali jinsi ulivyo, hata kama huna sikio moja, hata kama huna jicho moja au yote, hata kama huna mguu mmoja au yote kabisa, yeye anakupenda ulivyo.
Nimalize kwa kusema, jikubali ulivyo maana hukujiumba wewe hivyo ulivyo ni Mungu amekufanya uwe hivyo ulivyo. Ambaye hakukubali, ambaye ana mashaka na wewe, ambaye anaona kinyaa kuishi na wewe, huyo usimruhusu kwenye maisha yako. Hata kama umesubiri mume/mke kwa miaka mingi sana, achana naye kabisa hakufai, yupo wa kwako atakuja, atakupenda na wewe utampenda, atakukubali na wewe utamkubali alivyo kaakaa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.