Wanasema jifunze kwa waliofanikiwa vilevile naweza kukuongezea ni vyema pia ukajua walioshindwa walishandwaje. Ili usije na wewe ukaanza vizuri alafu ukashindwa kama walioshindwa.
Leo tujifunze pamoja kwa mtumishi wa Mungu Ayubu, nasoma habari zake zinanifanya nifunguke ufahamu wangu zaidi. Kwa jinsi nilivyokuwa nimemezeshwa baadhi ya vitu, sasa nimeviondoa rasmi baada ya kusoma habari za Ayubu.
Ninachoweza kukuambia, usiwe na shaka kumweleza Mungu na kumhoji kuhusu hali unayopitia. Usikae kimya tu huelewi Neno lake bado unakomaa tu, usikae kimya unaona wenzako wanafurahia neno la Mungu na kulielewa alafu wewe huelewi. Unapaswa kupaza sauti mbele za Mungu kumuuliza ni mpango wake wewe uwe hivyo au kuna eneo unakosea.
Utasema labda wao wanaelewa kwa sababu wameenda shule ya biblia, tunao watumishi wengi walio na nguvu za Mungu na wanaoichambua biblia kama walikuwepo wakati inaandikwa. Ila hawajaenda hata hiyo shule unayosema, japo sipangani na shule ya biblia nasema ni mhimu sana kama utapata nafasi hiyo nenda.
Lazima ukae chini umuulize Mungu kwanini wewe ni mtu wa kuumwa kila siku, na kuna watu hawajui mlango wa hospital zaidi ya kwenda kuwasalimia na kuwatia moyo wagonjwa mahospitalini.
Lazima umhoji Mungu kwanini wewe ni mtu wa kuhangaika tu kila siku bila mafanikio, kama ni mtu wake kwanini asikusaidie. Kama kuna sehemu unakosea si angekuambia, ni mangapi amekutendea na kukujibu, na kukutumia kwa wengine kutenda makubwa.
Usiogopeshwa na Mtu kuhusu kueleza uchungu wako mbele za Mungu, usijifunikefunike wakati moyo wako umejaa huzuni. Unataka ukaseme kwa nani kama sio Mungu wako, kusema maumivu yako mbele za Mungu sio kwamba umemwasi. Bado unamwamini na huna wazo la kumwasi, ila unachoumia moyoni mwako ni hali uliyonayo.
Kuna rafiki yangu mmoja tulikoseana, sasa wakati nataka kutoa ya moyoni ili kurekebisha hilo jambo lisije likajirudia. Yeye alitaka kuyamaliza mambo kwa kusema yaishe, binafsi nilikataa kabisa na kumwambia subiri niseme ya moyoni kisha nitahitimisha.
Binafsi huwa sina unafiki, eti kumwambia mtu haina shida tumalize wakati amenikera na najua nisipomwambia kesho atarudia yale yale na hatajua kosa lake. Nataka kusema nini hapa? Ninachosema ni kueleza haja ya moyo wako mbele za Mungu kwa kujiachia vizuri kabisa.
Ayubu ananipa shule kubwa sana katika tabu yake, anafika hatua anamuuliza Mungu kwanini aliruhusu azaliwe na wakati alikuwa ana uwezo wa kutoruhusu yeye azaliwe. Anamhoji Mungu kiasi kwamba leo ungesikiwa na watu wengine wangesema acha kunena maneno kama hayo mbele za Mungu.
Si mnafahamu kuwa kuna watumishi huwa hawataki tumwombe Mungu kwa njia ya machozi na vilio, lakini biblia inatueleza wazi watu wake wengi walimlilia Mungu kwa machozi mengi akawajibu.
Pamoja na Ayubu kuongea mengi mbele za Mungu, bado alikuwa anamjua vizuri BABA yake. Hata hoja alizokuwa anatoa zilikuwa zina nguvu kwelikweli, hebu tazama kama hii;👇🏾👇🏾
Lakini mambo haya uliyaficha moyoni mwako; Najua kuwa haya yamo nafsini mwako; AYU. 10:13 SUV.
Hebu kuwa huru mbele za Mungu kumweleza kinachokusumbua, kumweleza Mungu mambo yako inakupa nafasi ndani ya moyo wako, pia inakusaidia kupumua ndani ya moyo wako.
Mungu akubariki sana wewe uliyechagua fungu lililo jema la kujifunza Neno la Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.