Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, wakati mwingine tena Bwana ametupa kibali, tupate kushirikishana baadhi ya maneno ya Mungu kutujenga kiroho katika maisha yetu.

Upo wakati tunashindwa kuonyana kutokana na ukaribu wetu wa urafiki/undugu, unakuta mtu anaenda kinyume na maagizo ya Mungu unashindwa kumwambia. Ili kulinda undugu wenu usipotee unaona vyema kukaa kimya, huku akiendelea kutenda maovu.

Unapoendelea kumwacha mtu yule, hatajiletea tu madhara yeye, atasababisha wote mpate shida kubwa zaidi. Kwanza unakuwa na hatia mbele za Mungu kumwacha ndugu yako kufanya yasiyofaa, alafu humwambii acha kufanya hivyo.

Ile hofu ya Mungu iliyo ndani yako, itumie vizuri kuwarejesha wale wanaotaka kwenda kinyume na utaratibu wa KiMungu. Wakati mwingine tumesababisha uovu uingie ndani ya nyumba zetu kwa kushindwa kukemea wale wanaoleta huo uovu.

Unaona kijana mwenzako analeta picha mbaya kwa vijana wenzake, umekaa kimya husemi na wewe ni kiongozi. Alafu wengine wanatazama ile hali wanaona kumbe kufanya vile ni vizuri, taratibu unazidi kupanda mbegu ya uharibifu ndani yake.

Anatokea mshirika ametenda uovu/dhambi ambayo kila mmoja aliona, wewe kama kiongozi wa kanisa ukakaa kimya hukusema lolote. Jua pando lile la uovu, litaenda kuzaa matunda ya uovu zaidi, ikiwa hutokata hilo tawi la uovu lililochipuka.

Usiogope kumkanya nduguyo anayetaka kutoka nje ya utaratibu wa Mungu, kumwogopa kwako kunaweza kuleta madhara makubwa sana kwa familia nzima.

Labda nikutolee mfano huu unaweza kunielewa vizuri zaidi; una mtoto wako ambaye ni binti mdogo tu, akaanza tabia fulani mbaya mbaya. Walivyoona majirani zako walikuja kukuambia na kukuomba umkanye mwanao kuhusu tabia yake. Lakini hukuwasikiliza, ukajisemea moyoni wanamwonea mwanao wivu kwa sababu ya uzuri wake, ikatokea wakampinga. Badala ya kuwashukuru wamekusaidia kumkanya mwanao, ikatokea unamtetea kwa tabia yake na kuwatukana mbele yao kwa kumchapa mwanao.

Baada ya muda fulani binti yule atazidi kukua akijua kutenda kosa lile kumbe ni halali yake, maana anaona ukimtetea na akiguswa na majirani haupo tayari kuona ikitokea hiyo adhabu. Uwe na uhakika baada ya muda fulani atakuwa ni mtu aliyebobea katika eneo lile la uovu, na kumwondoa kwake hutoweza mpaka Mungu aingilie kati. Ndio maana ukisoma biblia yako unakutana na Eli ambaye hakuwakanya wanaye, kwa tabia zao mbaya. Kilichokuja kutokea ni pigo la Mungu juu ya Eli, kwa kosa ambalo alilitenda la kutowakemea wanaye kwa uovu wao.

Hapa nilikuwa najaribu kukupitisha mifano mbalimbali ili uweze kunielewa faida ya kumweleza ndugu yako aache uovu wake, na hasara ya kutomweleza ndugu yako aache uovu wake.

REJEA; Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya BWANA, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili. Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za BWANA, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia. 2 NYA. 19:9‭-‬10 SUV.

Epuka ghadhabu ya Mungu juu ya maisha yako kwa kumweleza ukweli aliyetenda baya alafu akaletwa kwako. Ili ujisalimishe na usije ukadaiwa damu yake mikononi mwako mbele za Mungu, unapaswa kumkanya juu ya tabia yake mbaya.

Shika hilo sana siku zote za maisha yako, usiogope kwa sababu ni ndugu yako, usiogope kwa sababu kufanya hivyo mtavunja uhusiano wenu na Mungu kwa sababu yake.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com