Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, muda mwingine tena wa kwenda kukushirikisha machache niliyojifunza siku ya leo.
Yapo makosa tunaweza kumkosea Mungu wetu, kukosea kwetu tunapaswa kutubu mbele za Mungu na kuacha yale tuliyotubia. Wachache huwa wanafanya hivyo pale wanapogundua wamekosea, na wengi huwa hatutubu mbele za Mungu.
Dhambi ina tabia moja usipoijutia na kuitubia mbele za Mungu, unaweza kuwa na tabia ya uzinzi/uasherati. Unapokosewa na huyo uliyekuwa unazini naye, utatafuta mwingine wa kwenda kupoza moyo wako, huyo naye akikuuzi unatafuta mwingine tena wa kulala naye.
Ndipo pale unapokutana na mtu anaitwa malaya, shida yake ipo ndani yake. Anafikiri shida ipo kwa anaolala nao kwa uasherati/uzinzi. Kumbe ndani yake ana shida hiyo.
Badala ya kuacha tabia mbaya, anazidi kuongeza foleni nyingine zaidi akifikiri atapata unafuu. Akijua atapata furaha kubwa kuwa na mwingine asiye na kero, kumbe shida yake anapaswa kuacha kulala ovyo na wanawake/wanaume.
Nimewahi kumsikia dada mmoja akisema, siwezi kuwa na mwanaume mmoja muda mrefu kwa sababu sikuzaliwa naye, nikimchoka nabadilisha mwingine. Kwanza kufanya mapenzi na mtu ambaye hajafunga naye ndoa ni kosa, anaona haitoshi anataka kuwa na wanaume wengine zaidi na zaidi.
Ndivyo ilivyo dhambi usipoitubia, itakutesa mwanzo mwisho, ni sawa na usipoutibu ugonjwa wa ukiambukiza. Utazidi kuenea maeneo mengine zaidi mpaka pale utapowekewa kinga ya kutoendelea kwa wengine.
Dada unapopata mimba ambayo hukupanga kuipata usikimbilie kuitoa, jua hayo ni matokeo ya dhambi. Unapaswa kutubu mbele za Mungu, na sio kuongeza dhambi juu ya dhambi.
Unapojikuta umeua mtu, na akatokea mtu mwingine akakuona. Usikimbilie kumuua yule aliyekuona ili kumaliza ushahidi. Huko ni kuongeza kosa juu ya kosa, unachotakiwa ni kutafuta namna ya kuepukana na jambo baya ulilolisabisha mwenyewe.
Hili tunaliona vizuri zaidi kwenye andiko la biblia, watu waliomkosea Mungu wakataka kuendelea kumkosea Mungu, wakazuiliwa kufanya hivyo.
Rejea; wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za BWANA, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli. 2 NYA. 28:13 SUV.
Hatia uliyonayo ni kubwa mbele za Mungu, usikimbilie kuongeza hatia nyingine tena, utamkasirisha Mungu mara mbili zaidi. Unapaswa kutuliza mawazo yako kujua namna gani utamwendea Mungu kumwomba toba kwa yale mabaya uliyomtendea.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
www.chapeotz.com