
Mtu akionekana hana huruma kwenye baadhi ya maeneo, mtu huyo anaonekana bado hajaokoka vizuri ama bado hajajazwa na Roho Mtakatifu.
Yatatengenezwa maneno juu ya huyo mtu ambayo yatamwonyesha hafai kabisa mbele za Mungu, na mbele za watu wengine.
Sababu kuu ni vile anavyofanya mambo bila huruma yeyote, vile anasukumwa kufanya ndani ya moyo wake. Ama vile ameagizwa ndivyo atakavyofanya vile vile.
Binadamu tumeumbiwa huruma ndani yetu, ama tunaweza kusema mtu akiwa na Yesu moyoni mwake. Mtu huyo lazima awe na huruma ndani yake, maana ni kitu ambacho Mungu amekiumba.
Sasa anapotokea mtu ambaye anafanya vitu bila kuonyesha huruma kwa mtu yeyote, yaani hata kwa wale ambao anafamiana nao. Mtu huyo huwa anatengeneza chuki kubwa sana kwa watu.
Pamoja na hayo, leo nataka nikuonyeshe kupitia maandiko matakatifu kuwa kuna wakati Mungu hataki uonyeshe huruma yako.
Kwanini kuna wakati Mungu hataki uonyeshe huruma yako? Mungu atakupa maagizo ya kwenda kushughulikia jambo fulani kwa watu. Na kukuambia usije kuonyesha huruma kwao, na ufanye kile ambacho amekuambia yeye.
Rejea: Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa BWANA, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo. KUM. 7:16 SUV.
Unaona hilo agizo la Mungu, kama hujawahi kusikia hili, ama kama hujawahi kusoma andiko kama hili unaweza ukapata picha mbaya juu ya mtu ambaye hana huruma kwenye baadhi ya maeneo.
Ikiwa ni mtumishi wa Mungu, ikiwa ni mwana wa Mungu, anafanya mambo fulani bila kuonyesha huruma na unamwona hana wasiwasi wowote.
Ule wasiwasi unaonyesha anamkosea Mungu haupo kabisa kwake, uwe na uhakika hilo jambo Mungu mwenyewe anahusika hapo.
Ujasiri wa watumishi wa Mungu kukemea dhambi bila kuangalia mtu usoni, ama bila kumwonea mtu aibu, ama bila kumwonea mtu huruma.
Eti kwa sababu fulani ambazo wengine wanaona asingekemewa, kwa mtu anayeongozwa na Roho Mtakatifu hilo haliwezi kuwa shida kwake. Wala haiwezi kuwa kizuizi kwake kushindwa kutekeleza lile agizo alilopewa na Mungu.
Usitafisiri watu kwa mawazo yako binafsi na ukatoa hukumu yako kwao bila kujua walichobeba ndani yao ni nini, ama bila kujua neno la Mungu linasemaje kuhusu hilo linalotokea.
Rejea: Wakati BWANA, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; KUM. 7:2 SUV.
Tumeona wana wa Israel wakipewa maagizo hayo na Mungu, hili lilikuwa taifa teule la Mungu. Ambapo na wewe leo Mungu amekuchagua/amekuita, hupaswi kwenda kinyume na yale aliyokuagiza.
Ukisikia Roho Mtakatifu anakuambia fanya hivi usionyeshe huruma yako kwa hao watu, hakikisha unafanya kama Mungu wako anavyotaka ufanye.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com