Kadri ninavyozidi kusoma Neno la Mungu hatua kwa hatua, nazidi kuona madhara ya mtu kushikilia mstari mmoja wa biblia au mistari michache ya biblia. Kuiona imemaliza kila kitu, haitaji mingine tena.
Pia nazidi kujifunza faida ya kujua maandiko matakatifu mengi, inasaidia sana kupanua ufahamu wa mkristo. Mtu anakuwa mwelewa zaidi ya yule anayeegamia mstari mmoja au michache tu, bila kujua maandiko mengine yanasemaje.
Kwanini nasema haya, haya yamekuja baada ya kujifunza Neno la Mungu katika kitabu cha Nahumu sura 3. Nimejifunza kitu cha tofauti kabisa, nilijifunza kutofurahi juu ya adui yako anapopatwa na mabaya.
Rejea: Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu. MIK. 7:8 SUV.
Lakini leo nimeweza kujifunza kumbe watu wanaweza kufurahia pale utakapoanguka, pale Mungu atakaporuhusu mabaya yakupate kwa kutokusikia kwako.
Watu watafurahi kupatwa kwako na mabaya, kwa sababu uliwatenda yaliyo mabaya. Kila mtu aliyebahatika kupita kwenye mikono yako, lazima aliondoka na kilio kichungu sana.
Wapo watu wa namna hii, watu wanaotenda wenzao mabaya, pamoja na kuonywa sana na jamii, hawakutaka kusikia. Pamoja na kuonywa sana na watumishi wa Mungu, hawakuta kusikia, inapofika wakati Mungu akaachilia mapigo yake kwao. Huwa kuna vicheko vingi sana vinakuwa kwao.
Hujawahi kuona kuna mtu alikuwa wanatendea watu mabaya sana, siku akipatwa na shida ngumu, shida inayomfanya asiwe na uwezo wowote wa kimwili. Watu hufurahi sana, utasikia afadhali bwana, huyu mtu ametutesa sana.
Inawezekana kabisa huyo mtu amepata labda ajali mbaya, ajali iliyopelekea kupoteza baadhi ya viungo vyake vya mwili. Badala ya watu kusikitika kwa kuumia kwake vibaya, watu watafurahi sana, na kuona kama vile mambo waliyokuwa wanafanyiwa yamefika mwisho.
Hujawahi kuona mtu fulani jambazi, aliyekuwa anasumbua watu sana, siku anaingia kwenye mikono ya askari wenye nguvu. Jambazi huyo akauawa, utasikia watu wanasema afadhali bwana ameuawa, ametusumbua sana.
Hujawahi kuona mtu alikuwa anawafanyia watu mabaya, ukasikia amehukumiwa kifungo cha maisha. Badala ya watu kumwonea huruma kwa maisha yake yote kuishia jela, watu wanapata amani moyoni kwa kifungo chake.
Watu hawa hawafanyi hivi kwa sababu ya chuki mioyoni mwao, watu hawa wanafanya hivi kwa sababu ya mambo mengi mabaya aliyokuwa anayafanya huyo mtu. Pamoja na kuonywa sana hakutaka kusikia, badala yake alizidi kutenda yaliyo mabaya.
Haya mambo yapo kibiblia kabisa, ndio inashangaza kukuta jambo kama hili lipo kibiblia ila unapaswa kufahamu biblia imebeba hazina kubwa sana ya maarifa. Ukiwa na muda wa kusoma na kutafakari vizuri, utakuwa sio mtu wa kawaida kawaida.
Rejea: Jeraha yako haipunguziki; jeraha yako ni nzito sana; wote wasikiao habari zako wapiga makofi juu yako; kwa maana ni nani ambaye uovu wako haukupita juu yake daima? NAH. 3:19 SUV.
Tunafundishwa nini hapa, Mungu anapotumia Neno lake kutuonya juu ya dhambi fulani tufanyayo, tunapaswa kuacha. Tunapokemewa na watumishi wa Mungu, na tunapoonywa na watumishi wa Mungu, tunapaswa kuacha matendo mabaya.
Kuacha kuwasikiliza watumishi wa Mungu wanaoisema kweli ya Mungu, na kuwa na shingo ngumu tunapokatazwa kufanya mambo mabaya. Siku Mungu akiachilia mapigo kwetu, kila atakayetuona atafurahia mabaya yaliyotupata.
Vizuri kufahamu haya na kuyafanyia kazi katika maisha yetu ya kila siku, kutofahamu kunaweza kutuletea shida ngumu sana.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.