
Yapo makosa yanaweza kufanywa na ndugu yako wa kimwili, au kiroho, kosa ambalo hata wewe huafikiani nalo kabisa kama mwana wa Mungu.
Unaweza ukawa unamweleza kila mtu, hata wale ambao sio ndugu zako wa kimwili au kiroho. Ukawa unawaeleza ubaya wa ndugu yako, au rafiki yako, au mzazi wako.
Unaweza ukaona ni sahihi kufanya hivyo ila ukweli ni kwamba unatoa nafasi ya kusemwa vibaya familia yako.
Hatakuwa peke yake tena yule aliyetenda dhambi/kosa. Atakuwa amewaunganisha wote kama familia kusemwa vibaya na watu wengine waliosikia habari za ndugu yenu.
Kwahiyo kuna mambo hata kama unaona aliyefanya mtoto wako, baba yako, mama yako, ama ndugu yako yeyote yule. Hupaswi kusambaza habari zake kwa watu wa nje.
Unaweza kupuuza hili, badala ya aibu kubaki kwa mtu mmoja. Inakuwa aibu ya familia nzima, inakuwa aibu ya kanisa zima, inakuwa aibu ya ukoo mzima, inakuwa aibu ya jamii nzima.
Fahamu hili jambo litakusaidia sana katika maisha yako ya kila siku, unapaswa kuwa makini sana na yale unayowaambia watu wengine.
Hili tunaliona kwa Daudi, baada ya Sauli kufa hakutaka habari zile kusemwa/kusambazwa kwa Wafilisti.
Rejea: Msiyahubiri mambo haya katika Gathi, Msiyatangaze katika njia za Ashkeloni; Wasije wakashangilia binti za Wafilisti, Binti za wasiotahiriwa wakasimanga. 2 SAM. 1:20 SUV.
Usiwape watu nafasi wafurahie kupitia shida yenu iliyowapata kama kanisa, au familia, au Taifa.
Mambo mengine mnapaswa kunyamaza au kukaa kimya, linabaki kwenu tu. Hata kama watu wengine watasikia, wabaki na sintofahamu ya kutopata taarifa kwa wahusika.
Nasisitiza juu ya hili, sio kila jambo baya lililotokea linapaswa kusambazwa kwa kila mtu. Mengine ni ya kunyamaza kimya kwa faida ya kanisa, au familia, au Taifa.
Baki/bakini nyinyi kama familia, au kanisa, au nchi mnaumia, au unaumia ila sio kuwaeleza, au kuwapa nafasi maadui kusikia kutoka kwenu/kwako.
Mungu akusaidie uweze kujua habari za kusambaza, na habari zisizo za kusambaza hovyo.
Yesu atusaidie sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81