Tumejikuta tukiishia kulaumu wengine, kwa sababu tulitegemea watufanyie mambo fulani katika maisha yetu. Lakini hawakutufanyia hayo tuliyotegemea kutoka kwao.

Tumejikuta tunakwama mambo mengi sana katika maisha yetu, kwa sababu tuliweka asilimia kubwa kwa watu fulani kuwa watatufanyia yale tuliyoweka matumaini kwao.

Tumejikuta tukiacha wokovu, kwa sababu ya watu fulani tuliowaamini sana wakamwasi Mungu. Nasi tukaona haina haja kuendelea na wokovu, kama tuliowaamini wameanguka dhambini.

Tumejikuta tukiacha wokovu wetu, baada ya wale tuliokuwa tunawategemea kutulea kiroho na kimwili kufariki Dunia. Mtu anaona kuendelea kumfuata Yesu Kristo haina maana tena kwake.

Mwanadamu mwenzako kuchukua nafasi ya Mungu wako, yaani unamtegemea kiasi kwamba unafika mahali unaona bila yeye huwezi kufanya chochote. Unaona kila kitu anaweza yeye tu, umefika mahali unaona Mungu hana nafasi sana kwako.

Mungu anasema kwamba, amelaaniwa mtu yule anayemtegemea mwanadamu mwenzake kuliko yeye.

Rejea: BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.YER. 17:5 SUV.

Tunaona kumbe kumtegemea mwanadamu ni laana, maana unakuwa unamtegemea mtu ambaye na yeye anapaswa kumtegemea Mungu. Ulivyo huelewi mwanadamu mwenzako anachukua nafasi ya Mungu moyoni mwako. Unaacha kumtegemea Mungu wako, unakuwa unamtegemea binadamu mwenzako, huko unakuwa unafanya machukizo mbele za Mungu.

Mtu anayemtegemea Mungu kwa kila jambo katika maisha yake, anayempa Mungu nafasi ya kwanza kuliko mambo mengine. Mtu anayetoa muda wake mwingi kutulia na kusikiliza Mungu anasema nini juu ya maisha yake ya kazi, ndoa, biashara, familia, masomo, na malengo yake.

Mtu wa kumsikiliza Mungu, Mtu wa kumtegemea Mungu, mtu anayemtumaini Mungu wake siku zote. Mtu yule amebarikiwa sana na BWANA, tena ni heshima kubwa Mungu anapombariki mtu wake.

Rejea: Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake.YER. 17:7 SUV.

Kwanini usitafute baraka hizi za Mungu wako? Kwani kumtegemea Mungu isapavyo unapaswa kutoa shingapi? La hasha hakuna gharama yeyote ile unaweza kupoteza kwa Mungu wako.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081