Kusitasita kwa wengi kufanya mambo makubwa, kuogopa kujitokeza kufanya kitu ambacho Mungu amempa uwezo ndani yake, kukosa ujasiri wa kusimama vizuri. Ni pale mtu anapotaka watu wamkubali kwanza, pale anapotaka wazazi wake wakuabaliane naye kwanza.

Mwanafunzi hawezi kusomea kitu anachopenda ndani ya moyo wake, mpaka akaulize wazazi kuhusu kile anachotaka kusomea, mpaka akajue mtazamo wa ndugu zake uko vipi juu ya kile anataka kwenda kusomea.

Binti ameokoka vizuri, anajitambua vizuri ila hana maamzi ya kujitegemea mwenyewe, kuamua juu ya mume wa maisha yake anayepaswa kuja kuishi naye. Hadi wazazi wake na ndugu zake wamkubali wote huyo mwanaume, hadi aombe apate ruhusa ya kuolewa na mwanaume anayemwona ni sahihi kwake.

Na kama mwanaume huyo sio chaguo la wazazi/ndugu hataweza kuolewa naye, haijalishi huyo mwanaume alipewa au alikutanishwa na Mungu. Wanaweza kuvuruga uhusiano wao kutokana na wazazi/ndugu hawajamkubali huyo mwanaume.

Kuna mtu anaogopa kuokoka, yaani kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, kwa sababu hajamwomba ruhusa baba/mama yake, kwa sababu hajamwomba ruhusa mume wake.

Kuna mtu hawezi kufanya kazi anayoipenda, hadi ameenda kwanza kuomba ruhusa kwa ndugu zake, wakimwambia hiyo kazi mbaya, hataifanya kabisa. Hata kama moyoni mwake anasikia msukumo wa kuifanya hiyo kazi, maana anaona angeifanya kwa moyo wa kupenda.

Kuna mtu hawezi kuchukua hatua ya kusoma Neno la Mungu, hadi akaombe kwanza ruhusa akubaliwe, akikataliwa kusoma Biblia, naye anakubaliana na hilo. Uamzi wa kujitegemea hana, anachotaka yeye ni kupata kwanza ruhusa kutoka kwa watu wake wa karibu.

Kuomba ruhusa sio vibaya, wala kutaka kuwataarifu watu kuwa unataka kufanya jambo fulani sio vibaya. Changamoto inakuja pale ambapo huna uwezo wa kubaki na msimamo wako, huna uwezo wa kukataa kile kilicho kinyume na mapenzi ya Mungu.

Mfano, kwenu hawajaokoka wote, alafu unasikia msukumo wa kuokoka, unahairisha kwanza mpaka ukawaeleze ndugu zako juu ya uamzi wako unaotaka kuchukua. Majibu utakayokutana nayo yanaweza kukuondoa kabisa kwenye mpango wako wa kuokoka.

Yapo mambo unapaswa uchukue maamzi mwenyewe, watu wenyewe watapata taarifa mbele ya safari, na watakuelewa vizuri mbele ya safari. Kikubwa uwe humkosei Mungu, bali uwe unamletea Mungu utukufu, hata kama kuna baadhi ya watu hawataki kukuelewa. Wapo watu Mungu atawainua watakaokuelewa vizuri.

Tunajifunza kwa mtu mmoja aliyetaka kufuatana na Yesu Kristo, akamwomba ruhusa ya kwenda nyumbani kuanga kwanza. Yesu alimwambia moja kwa moja hilo halifai.

Rejea: Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu. LK. 9:61‭-‬62 SUV.

Hebu fikiri ni mangapi umekwamishwa kwa sababu ulitaka ndugu zako wajue kwanza, walivyojua wakageuka kizuizi kwako. Hadi leo umebaki kwenye kizuizi, na lile ambalo ulikusudia kulifanya, ulishindwa kulifanya.

Mungu wetu ni mwingi wa rehema, anaweza kukusamehe ukitubu, ukaanza upya. Maana anasema mtu anayetaka kumfuata, alafu akataka akawaage wa nyumbani mwake kwanza, hafai kwa ufalme wa Mungu.

Usiwe mtu asiyefaa, umeamua kuambatana na Yesu Kristo fanya hivyo bila kuangalia wangapi wanamkataa, wangapi wanakubaliana na wewe, wangapi wamekuunga mkono.

Mungu amekupa uwezo mkubwa wa akili, zitumie sawasawa ila usizitegemee tu akili zako mwenyewe. Utaona ukifanikiwa kiroho na kimwili pasipo kuyumbishwa na watu kimaamzi.

Umesoma somo hili hadi mwisho, hongera sana, uishie hapa, karibu sana kwenye darasa la kusoma Neno la Mungu kila siku. Darasa hili lipo WhatsApp group, ili uunganishwe, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda +255759808081.(tumia wasap tu)

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081