“Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari”, Mwa 13:10 SUV.
Kisa hiki cha Abramu na Lutu kinatupa funzo kubwa sana sisi tuliopo siku za leo, funzo ambalo ukilichukulia kwa uzito na umakini litakusaidia katika maisha yako yote ya kimwili na kiroho.
Lutu aliona bonde lenye maji na lenye kupendeza kwa kulisha mifungo yake na kuishi humo. Lakini Mungu aliona Sodoma na Gomora walikuwa ni wabaya na wenye kufanya dhambi nyingi sana mbele zake.
“Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA”, Mwa 13:13 SUV.
Wakati Lutu anaona ni mji mzuri wa kuishi, Mungu alikuwa na mipango mingine kabisa ya kuuteketeza kwa moto. Ule upande wa Abramu ambao ulionekana sio mzuri sana ndio mji ambao Mungu alikuja kuustawisha vizuri sana.
Yapo mambo tunayaona ni mazuri sana kwa macho ya nyama, kumbe Mungu hayaoni kama tunavyoona sisi, Mungu anaona tofauti kabisa na sisi wanadamu, na wakati mwingine hatutaki kumsikiliza yeye kwanza.
“Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo”, 1 Sam 16:7 SUV.
Tunaweza kuchagua maeneo mazuri sana ya kufanya biashara, kumbe hayo maeneo hayana muda mrefu yatapotezwa kwa sababu ya mambo mabaya yanayofanyika katika maeneo hayo.
Unaweza kumwona mtu kwa macho ni mzuri wa sura na mali nyingi, anafaa kuwa mwenzi wako wa maisha, kumbe Mungu anaona jambo tofauti kwake na hataitachukua muda mrefu ataondolewa duniani au mali zake na uzuri wake utaondolewa.
Macho yetu ya nyama Mungu ametupa na tunapaswa kuyatumia vile tupendavyo ila hatupaswi kusahau nafasi ya Mungu katika maisha yetu, tusipofanya hivyo tunaweza kujikuta tumeingia kwenye maeneo ambayo yatatuletea majuto katika maisha yetu.
Vizuri kwenda mbele za Mungu kwa kumwomba na kusikiliza sauti yake kabla ya kufanya maamuzi makubwa, tunaweza kujiona tuna uwezo sana na elimu kubwa ya kutambua mambo lakini mwisho wake tukaangukia kwenye eneo baya.
Tumpe Mungu nafasi kubwa katika maisha yetu kama ilivyokuwa kwa Abramu, yapo mambo watu wengine wanaweza wasione ila wewe ukasaidiwa na Roho Mtakatifu kuyaona na kuyaepuka kuyafanya katika maisha yako.
Wakati wengine wanakimbiza na mambo ya dunia hii, Mungu anakuonya usifanye kama wengine, wale wanaosikia sauti yake wanakuwa salama na wale ambao hawakusikia sauti yake wanakutana na madhara makubwa katika maisha yao.
Mungu akusaidie macho yako ya ndani yatiwe nuru maana haya ndio huona kwa usahihi pasipo tamaa wala upendeleo wowote, hakikisha uhusiano wako na Mungu ni mzuri na ujikabidhi mbele za kwa mambo yako yote.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Samson Ernest
+255 759 80 80 81