Tupo Duniani, Dunia yenye kila rangi, Dunia yenye watu wa aina tofauti tofauti, wenye kujivuna kwa nguvu za mali zao, wenye kujivuna kwa nguvu za miungu yao.

Watu wa namna hii wanapokutana na watu wanyonge wasio na mali, lakini wana Mungu wa kweli ndani yao. Hutaka kutumia nafasi hiyo kuwaonea watu hawa kwa kutazama madhaifu yao kimwili.

Kweli kuna watu wanatisha watu, tena wanakuambia utanifanya nini wewe maskini mkubwa usiye na kitu. Mungu wako angekuwa anaweza angekusaidia kukutoa kwenye umaskini ulionao.

Ukiambiwa maneno kama hayo, kama hujaiva vizuri kiroho, lazima wasiwasi ukiingie. Na lazima uone huwezi tena kushinda vita ile.

Tena mtu mwenyewe anaweza kumtukana Mungu wako, akiamini nguvu aliyonayo ni kubwa. Ndio anaona ni kubwa kwa sababu amefanya matukio mengi ya maangamizo, hakuna kilichomhangaisha.

Anajua na wewe unayemtengemea Mungu wa kweli, anaweza kukufanya chochote usiweze kujiokoa kwa lolote.

Hili tunajifunza kwa mfalme wa Ashuru, ambaye aliitwa Senakeribu, alijiona ana nguvu sana. Alitumia nguvu zake kumtisha mfalme Hezekia, na akamtajia mataifa aliyoyaangamiza.

Mfalme Hezekia baada ya matisho ya mfalme Senakeribu kutaka kuangamiza Yuda na Yerusalem ili atawale yeye hiyo miji. Hezekia alimwendea Mungu wake aliye hai.

Hebu tuone Mungu alimwambiaje mfalme Hezekia, ili tuweze kuona nguvu ya Mungu wa kweli tunayemtegemea kila siku.

Rejea: Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; BWANA asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana. ISA. 37:6 SUV.

Sijui kama umeona vizuri hilo andiko, ni andiko lenye nguvu sana kwa mtu ambaye anamtumikia Mungu wa kweli, kwa mtu anayemtegemea Mungu wa kweli.

Mungu anakuambia leo, Usiogope, haijalishi kuna taarifa gani umezipokea kutoka kwa maadui zako, Mungu anasema Usiogope matisho yao.

Mungu alisema maneno haya kwa mtumishi wake, ndiye Mungu uliyenaye wewe hata sasa, ndio unaye ndani yako. Hupaswi kuwa na mashaka yeyote yale juu ya maisha yako.

Acha wakutishie wanavyojua wao, we nenda mbele za Mungu, ndio nenda mbele za Mungu. Mweleze Mungu jinsi gani unahitaji msaada wake.

Nimependa maombi haya ya mtumishi wa Mungu Hezekia, hebu tusome tufahamu zaidi;

Rejea: Tega sikio lako, BWANA, usikie; funua macho yako, BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao, na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu. Basi sasa, BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako. ISA. 37:17‭-‬20 SUV.

Kilichofurahisha hapa kwa mtumishi huyu, ni kukiri aliyoyafanya mfalme Senakeribu, baada ya hapo akasema pamoja na kuangamiza mataifa mengi. Aliangamiza mashamba yao na miungu ambayo ni kazi ya mikono ya mwanadamu.

Ndani mwako unapenda kujifunza Neno la Mungu kila siku kwa kusoma, na una smartphone yenye uwezo wa kuwa na whatsApp. Unakaribishwa sana, wasiliana nasi kwa namba hizo hapo chini.

Mungu akupe kuona haya, ili ujasiri wa kiMungu uwe ndani yako siku zote.

Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081