Vijana wengi au watu wengi hili hulipuuza na kutazama hali nzuri ya anayetaka kumuoa au kuolewa naye.

Mara nyingi nimekuwa nikiwaambia vijana, “kuna dhahabu zimejificha kwenye tope”, hadi kuibaini unahitaji uwe na utulivu wa kiroho na uwe na mahusiano mazuri na Mungu.

Wapo wanaume au wanawake, ukimwona kwa jicho la nyama na hali aliyonayo au maisha anayoishi kwa sasa. Unaweza kumwona sio wa viwango vyako kutokana na hatua za kimaisha ulizofikia.

Wengine hawana hatua yeyote waliyopiga ila wamejiweka katika hali ya juu, kuna kundi hawawezi kukaa nao na wakateta jambo muhimu la maisha.

Kuna picha ya Rais aliyetangazwa jana Kenya, picha hii inatembea sana kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha Ruto na mke wake.

Ukimwangalia Ruto wa kipindi hicho huwezi kuwa na matumaini ya leo angekuwa Rais wa Kenya (hata kama hajaapichwa lakini ni Rais mtarajiwa) na ukimwangalia na mke wake alivyokuwa kipindi hicho usingedhania leo angekuwa mke wa Rais.

Huo ni mfano tu, ipo mifano mingi sana ya watu waliokuwa na maisha ya kawaida sana ila Mungu amewainua sana na huwezi kuamini kama ni wale wa miaka 10 au 20 au 30 iliyopita.

Vijana au wazazi hupenda kuona watoto wao wakioa wanawake au wakiolewa na wanaume wenye hali nzuri za kimaisha ya mwili (kiuchumi)

Sipingi wala sikatai hilo, hatari ninayoiona katika hili ni kwamba wengi hawaangalii kusudi la Mungu. Wanaangalia mtu ana nini, maisha yake kiuchumi yapo vipi?

“Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako”, Mit 3:5‭-‬6 SUV.

Narudia sipingi vijana au wazazi kuangalia hayo ila kama tutaangalia hayo kwa kutegemea akili zetu na kusahau usahihi wa mtu tunayemhitaji katika maisha yetu. Tutajikuta tunakuwa na ndoa za ajabu ajabu, ambazo zina matukio mengi ya aibu na kuumiza.

Wapo watu wanaonekana wamechoka sana, sio kana kwamba ni wavivu na hawapambani, kuna watu hata vaa yao haieleweki, hawajui kupangalia rangi za nguo na hawana muda wa kukimbizana na fasheni mpya za nguo.

Wasiojua na wasio na jicho la tatu, lile jicho la Kimungu watawachukulia kawaida, hawataona kitu ambacho ni cha thamani kwa wale watu. Watu ambao miaka 10 au 20 au 30 mbele watakuwa ni watu wa viwango vya juu kiroho na kimwili.

Kusudi la Mungu linaweza lisitimie kwa mtu ambaye atapata mwanaume au mwanamke asiye sahihi kwake, wapo watu wameharibikiwa maisha yao kwa sababu walikutana na watu sio sahihi.

Wachungaji au wazazi watakuruhusu kuoa au kuolewa na unayemtaka wewe ila fahamu ya kwamba maisha yatakuwa yako na mwenzi wako. Maumivu na mateso utakayokutana nayo ndugu zako wanaweza wasijue ila wewe ndio utakuwa unajua.

Ninachoweza kukushauri kijana kwenye eneo la mahusiano na unapotaka kuchagua mtu wa kuishi naye, hakikisha unaruhusu mapenzi ya Mungu katika uchaguzi wako.

“Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi”, Ebr 10:36 SUV.

“Walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke”, Lk 22:42(b) SUV.

Omba Mungu akusaidie, kuwa na neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, usiwe na parapara katika kuchagua na kufanya maamuzi yasiyo na Mungu ndani yake ya yule unayetaka kuishi naye.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081