“Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake”, Rum 14:1 SUV.

Huko Rumi waamini waligawanyika katika vyakula na siku za kusali.

Walihukumiana kwa vyakula walivyokula na kuhusu vile vyakula ambavyo hawakupaswa kula, na kuhusu siku za kumwabudu Mungu.

“Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe”, Rum 14:5 SUV.

Mtume Paulo akaliweka sawa jambo hili, akawaambia hakuna shida mtu kula chakula fulani na nyama.

Akawaeleza wazi kuwa suala la vyakula sio la kimaadili bali ni mtazamo wa mtu binafsi, ale nini na asile nini.

Siku za leo bado hili jambo lina utata kwa baadhi ya watu, wapo wanaona ni sahihi kula nyama ya mnyama fulani na wengine wanaona sio sawa na ni dhambi.

Ukweli ni kwamba hakuna dhambi yeyote anayofanya mtu kwa kula nyama ya mnyama fulani au chakula fulani.

Yule ambaye anaona ni dhambi kutokana na mtazamo wake asimhukumu yule ambaye anakula, na anayekula asimhukumu yule asiyekula.

“Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga. Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali”, Rum 14:2‭-‬3 SUV.

Imani yangu au mtazamo wangu unaniambia kula samaki fulani ni dhambi au kula nguruwe ni dhambi au kula sungura ni dhambi, basi nibaki hivyo na sio kuwaona wengine wanatenda dhambi.

Na Mimi ambaye naona kula chakula fulani au kinywani fulani sio dhambi, basi nisiwahukumu wale ambao hawatumii hivyo vitu na niliwalazimishe wavitumie kama ninavyovitumia mimi.

Vipo vitu sio dhambi ila mitazamo yetu kutokana na mafundisho tuliyopata au kutojua neno ipasavyo au kulifasiri isivyo sawasawa, tumejikuta tunaona vitu fulani ni dhambi na wengine wanaona sio dhambi.

“Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi”, Rum 14:14 SUV.

Tunapofika eneo kama hilo kila mmoja asimhukumu mwenzake, ukiona mwenzako anaona dhambi basi usibishane naye kupita kiasi, wale usitumie hicho kitu mbele yake.

Tuchukuliane kutokana na viwango vyetu vya imani, imani yako ikiwa juu msaidie yule aliye na imani iliyo dhaifu. Na wewe uliye na imani dhaifu japo unaweza usijue sana, ukubali kuna mambo bado hujui na unahitaji kujifunza.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081