Mtumishi wa Mungu anayeisema kweli ya Mungu, anayekemea dhambi, anayesema acheni dhambi. Haiwezi kuwa na uso wa tabasamu ikiwa maneno hayo anayoyazungumza msukumo wake unatoka ndani ya moyo wake.
Huwezi kumkuta mtumishi wa Mungu ana uso wa aibu, ikiwa amepewa agizo na Mungu wa kuwaambia watu habari zake. Lazima umkute anazungumza maneno yanayotoka ndani moyo wake, tena ana uhakika na kile anasema.
Wengi wetu tukishaona mtu wa Mungu anaongea akiwa amekunja/amekaza uso, huwa tunaanza kumwona mtu mbaya. Bila kujua kinachomfanya awe na uso uliokaza ni ule msukumo ulio ndani yake, kwa lugha nyingine tunaweza kusema hasira ya Mungu imewaka juu ya maovu ya mwanadamu.
Unaposikia mtumishi wake anahubiri habari za kumgeukia Mungu, usifikiri anasema tu. Mungu anamtuma aseme hayo, sio kusema tu, akaze uso wake anapozungumza ujumbe wake.
Kama huwa hupendi kuona mtu wa Mungu akiwa na uso mkavu akiwa anazungumza habari za watu kumgeukia Mungu. Uanze kufahamu kuanzia sasa, kuwa hilo ni agizo la Mungu aliloweka ndani ya mtumishi wake.
Mtumishi wa Mungu hawezi kuwa na uso wa aibu, wala hawezi kuwa na maneno ya kukurembaremba pale anapopewa agizo na Mungu. Unaweza kumchukia mtumishi wa Mungu anavyokemea dhambi ila unapaswa kujiangalia mwenyewe kwanini unakuwa na chuki naye.
Shetani anaweza kukupandikiza chuki kwa watumishi wa Mungu wanaoisema kweli yake, ili usipate nafasi ya kuelewa kile wanasema. Maana ni kawaida kabisa unapokuwa na chuki na mtu huwezi kumwelewa kile anasema juu ya maisha yako.
Unapaswa kuwa makini sana kwa hili, Mungu anaweza kutumia ukali kukuonya kuhusu tabia yako mbaya. Ukaona ni Mungu gani anasema na wewe kwa ukali wa namna hiyo, ukiona Mungu anasema nawe kwa ukali kupitia watumishi wake. Uwe na uhakika alishakuonya sana kwa upole, uwe na uhakika alishatumia walimu wake kukufundisha taratibu na kwa upole ila hukuwaelewa, wala hukutaka kuwasikia.
Tunajifunza hapa Mungu alivyomwambia nabii Ezekiel akaze uso wake juu ya Gogu, ikiwa Mungu alimwambia mtumishi wake akaze uso. Unapataje shida unapoona watumishi wengine wanasema habari ambazo Mungu hapendi kuziona kwako?
Rejea: Mwanadamu, kaza uso wako, umwelekee Gogu, wa nchi ya Magogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali, ukatabiri juu yake. EZE. 38:2 SUV.
Hili linatufunza hata katika maisha yetu ya kila siku, mtoto wako uliyemzaa hupaswi kumlea kizembe. Lazima kuna wakati utamkazia uso, kuna tabia mbaya anataka kuifanya yake, utapaswa kuikemea kwa nguvu zote.
Usichekee uovu wa aina yeyote ile, unapoona watu wanacheza na wokovu wako. Lazima uwakazie uso wako au jicho lako, ipo gharama ya kutoka kwa shetani na kuwa mtoto wa Yesu Kristo, alafu anatokea mtu anataka kuharibu maisha yako ya wokovu unakuwa unacheka naye!!
Dada lazima ufike mahali ukaze uso wako, usicheke na kaka/baba anayetaka kucheza na maisha yako. Umekombolewa kwa gharama kubwa sana, usicheze na Maisha yako ya wokovu, simama Kisawasawa.
Kaka ufike wakati usicheze na maisha yako ya ujana, fika mahali ukaze uso wako pale unapoona vijana wenzako wanataka kukuingiza kwenye uovu. Kijana aliyeokoka lazima awe makini anapokuwa na watu wasiomjua Kristo.
Mama/baba usicheze na ndoa yako, kaza uso wako pale unapoona kuna jambo lisilo la kawaida. Usiwe mpole wa kupitiliza, usiwe na aibu juu ya adui wa ndoa yako. Simama kisawasawa unapoona hali fulani kwenye maisha yenu ya ndoa, hasa pale Mungu anapokusemesha juu ya ndoa yako.
Nimekupitisha kwenye andiko takatifu uweze kuona ni jinsi gani unapaswa kukaza uso kulivyo, huenda ulikuwa unaona kukaza uso wako ni kumtenda Mungu dhambi. Kuanzia sasa utakuwa unaelewa kwanini huwa kuna watu wanafanya hivyo.
Ukitaka kuelewa vizuri, mwangalie askari anayesimama nyuma ya rais, huwezi kumkuta anacheka cheka ovyo. Huwezi kumkuta anatabasamu ovyo, maana yupo kazini, kama kuna mtu ana nia mbaya juu ya mkuu wake ni rahisi kumbaini.
Yapo mengi sana ya kukazia uso au macho yako, nimekupitisha machache uweze kuona umhimu wa hili jambo. Kaza uso wako kwenye maeneo yako yote, yaani kimwili na kiroho. Usiwe mtu wa kupuuza mambo madogo madogo yenye nia mbaya kwako.
Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081