Unaweza kujiuliza inawezekana vipi mtu akajenga nyumba nzuri, tena ya gharama kubwa, alafu asikae ndani yake au asiishi ndani yake.
Unaweza kujiuliza inawezekana vipi mtu akalima shamba, sio kulima tu, akapanda na mazao mazuri juu yake. Alafu huyo mtu asiweze kula matunda mazuri ya kile alichopanda shambani mwake.
Kama hujui haya, leo naenda kukufahamisha, utaelewa vizuri kabisa kwanini niandike kichwa cha somo cha namna hiyo.
Unaweza kuhangaika miaka mingi sana kujenga nyumba nzuri, ukafika mahali ukaimaliza hiyo nyumba yako. Lakini cha ajabu hiyo nyumba usikalie/usiishi ndani yake, ikakaliwa na watu wengine kabisa.
Sio kwamba umeona haifai kukalia/kuishi, unakuwa umeshakufa, unawaachia watoto wako au ndugu zako. Bila shaka hili umeliona kwa watu wengine, wanajenga nyumba nzuri, wanahamia humo, unashangaa baada ya muda mfupi kuhamia anafariki.
Unaweza ukalima shamba, ukapanda mazao yanayofaa kwenye ardhi ile au udongo ule, si unajua si kila ardhi inafaa kupadwa zao fulani. Nasema hivi; huwezi kupanda mhogo kwenye matuta ya mpunga, alafu ukavuna.
Utashangaa pamoja na kupanda sehemu nzuri, pamoja na mvua kuwepo za kutosha, pamoja na kupiga dawa vya kutosha ili wadudu wasiharibu mimea yako, pamoja na kuweka mbolea ya kutosha. Ukashangaa mimea yote uliyopanda shambani, ikazaa mapooza.
Ukienda kwa jirani yako, mazao yake unakuta yapo vizuri, unaweza ukasema labda umeuziwa mbegu feki. Unaweza kuwaza mengi, unaweza kufikiri labda umezidisha kiasi cha mbolea, yaani unaweza ukapata mawazo mengi sana.
Vilevile unaweza kupanda vizuri na mazao yakatokea, ila wadudu au wanyama waharibifu, wakaharibu mazao yako yote, ukaambulia sifuri.
Usipojua hiyo shida ipo kiroho, unaweza kuhangaika sana, msipojua hayo ni matokeo ya kufarakana na Mungu wenu. Mnaweza kuhangaika sana na wataalamu wa kilimo, mkashangaa matokeo yanakuwa yale yale.
Sababu ya uovu, ardhi haitatoa mazao, sababu ya uovu, utajenga nyumba, lakini hutaikalia hiyo nyumba. Dawa ya kuepuka haya yasikupate, ni kutengeneza uhusiano wako na Mungu.
Ukishatengeneza uhusiano wako na Mungu, kwa kutubu maovu yako uliyomtenda, unaachilia kibali hadi kwenye nyumba yako, unaachilia kibali kwenye ardhi unayolima na kuishi.
Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu haya ninayokueleza hapa;
Rejea: Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi. ISA. 65:21-22 SUV.
Kwa mjibu wa mistari hii miwili, inaonekana wazi kabisa huko nyuma hawa watu walikuwa wanajenga nyumba zao, lakini walikuwa hawakai ndani yake. Inaonekana walikuwa wanalima mazao mazuri, lakini walikuwa hawavuni kile walichopanda. Lakini baada ya kumrudia Mungu wao, aliachilia baraka kwao.
Ili ufurahie matunda ya kazi ya mikono yako, unapaswa kuwa na uhusiano mzuri na Mungu wako. Unapaswa kuokoka, unapaswa kuachana na mambo yanayomkosea Mungu wako.
Ukiona mambo yako hayaendi vizuri, kaa chini uangalie uhusiano wako na Mungu, je, upo sawa? Kama haupo sawa, tengeneza uhusiano wako na Mungu wako, usiwe na shingo ngumu utaangamia.
Hili litumie kwenye maeneo yako yote katika maisha yako, utaona mafanikio yakiwa upande wako.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081