Unaweza ukawa unawapenda sana watoto wako ila inapofika suala la matendo mema mbele za Mungu, kila mmoja anabeba furushi lake.

Unaweza ukawa unampenda sana mzazi wako ila inapofika suala la hukumu, Mungu atamhukumu kila mmoja sawa sawa na matendo yake.

Hakuna ujumla kwa mambo ya Mungu, kama unatenda dhambi ukifikiri unamkomoa mzazi wako. Ujue unajidanganya mwenyewe, elewa mzazi wako naye atahukumiwa sawa sawa na matendo yake.

Kama unatenda dhambi zako kwa siri, ukifikiri unamficha mke/mume wako. Siku ya hukumu ya Mungu utahukumiwa peke yako na sio na mke/mume wako.

Haijalishi una marafiki wengi sana wanaomjua Mungu, haijalishi una marafiki wengi sana wanaoishi maisha matakatifu. Haijalishi una wachungaji, manabii, mitume, wainjilisti, na walimu wengi sana unaojuana/unaofahamiana nao. Hiyo haiwezi kukupa wewe tiketi ya kuingia peponi.

Kama umejificha kanisani huku unatenda dhambi, wenzako wakawa wanaishi maisha ya kumpendeza Mungu wao. Usifikiri upo salama, elewa kila mmoja atahukumiwa sawa sawa na matendo yake.

Kuokoka kwa mwingine isikupe jeuri wewe, maisha matakatifu ya mwingine hayatakupeleka mbinguni, kila mmoja ataingia mbinguni kwa matendo yake mwenyewe.

Usije ukasema bora mzazi wangu ameokoka, haina haja ya wewe kuokoka, ukifikiri utaingia mbinguni kwa mgongo wake. Kama unawaza hivyo, hayo mawazo achana nayo kabisa, hakuna mbingu ya kupitia migongo ya wengine.

Haya ninayosema, Mungu aliyathibitisha mwenyewe kwa kinywa chake, hebu soma mwenyewe hapa;

Rejea: Wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU. Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao; wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa. EZE. 14:14‭-‬16 SUV.

Mungu anasema wakiwepo wenye haki wake watatu, ambapo kipindi hicho aliwazungumzia Nuhu, Ayubu, na Daniel, watajiokoa nafsi zao wenyewe. Wala hawatawaokoa watoto wao, yaani kila mmoja atajiokoa kwa matendo yake mwenyewe.

Hutaingia mbinguni kwa mgongo wa mchungaji wako, wala hutaingia mbinguni kwa mgongo wa mzazi wako, wala hutaingia mbinguni kwa mgongo mke/mume wako. Kila mmoja ataingia mbinguni kwa matendo yake mwenyewe.

Simama kwa miguu yako mwenyewe, usiangalie wingi wa watu wanaotenda dhambi na wewe ukatamani kuungana nao. Hata kama Dunia nzima itamwacha Mungu, wewe ishi maisha ya kumpendeza Mungu wako.

Mungu atusaidie sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.