Yakobo alichunga miaka saba kwa mzee Labani ili ampate Raheli kuwa mke wake. [Mwanzo 29:18_20].
Siku anataka kukabidhiwa Raheli, badala yake alibadilishiwa mke anayempenda akapewa Lea asiyempenda yeye. [Mwanzo 29:21_25]
Lengo la Yakobo ilikuwa ampate mdogo wake Lea ambaye ni Raheli, akaambiwa tamaduni haziruhusu kuoa mdogo na kumwacha mkubwa. Akashauriwa aongeze miaka mingine saba ili ampate kipenzi chake Raheli, kwa upendo aliokuwa nao kwa Raheli aliongeza hiyo miaka saba. [Mwanzo 29: 27_30]
Yakobo alimwona Raheli anafaa kuolewa na yeye, na ni mzuri sana kuliko dada yake Lea. [Mwanzo 29: 17]

SWALI LA MSINGI KWAKO.
1. Kinachokufanya ulalamikie mahari kubwa huwezi kuoa ni nini? Wakati Yakobo alitoa gharama ya miaka 14 kumpata Raheli.
2. Anayekuambia hakuna uchumba wa muda mrefu we oa/olewa haraka haraka ni nani? Wakati Yakobo alikaa kwenye uchumba miaka 14.
3. Anayekudanganya kulazimisha kuolewa/kuoa asiyekupenda, atakupendea ndani ya ndoa ni nani? Wakati Lea pamoja na kuchomekewa kwa lazima kwa Yakobo, bado hakupendwa kama Raheli.
4. Anayekudanganya ukioa mwanamke mzuri wa sura na umbo atakutesa sana, ni nani? Wakati Raheli alikuwa mzuri wa sura na umbo lakini hakumtesa Yakobo.
5. Wazazi kukulazimisha uoe/uolewe na mtu usiyempenda/asiyekupenda unafikiri ni kutimiza haja ya wazazi wako au kujiletea matatizo wewe mwenyewe? Wakati tunaona Lea akiingizwa kwa Yakobo kinyume na makubaliano. Na akikazana kumzalia Yakobo watoto ili apendwe lakini haikuwa hivyo.

Ushauri wangu kwako, usiyachukulie haya mambo kwa kawaida, mshirikishe Mungu, chukua/chukuliwa na yule moyo wako unapenda. Kama ni changamoto za kupata mke zilianza enzi za Yakobo badala ya kupewa Raheli alipewa Lea. Pamoja na hayo Yakobo hakukata tamaa kumsubiri yule aliyempenda.

Leo wewe umeachwa na mchumba wako unakata na tamaa ya kuoa/kuolewa, ungekutana na Yakobo si angekucheka sana. Yeye hakuona kitu kuongeza kipindi kingine cha miaka saba ili ampate yule wa moyo wake.

Leo unasumbuliwa na mahusiano kidogo unaacha na wokovu, kisa aliyekusumbua alikuwa anasema ameokoka, ungekutana na Yakobo angekuambia huna uvumilivu.

Nikutakie mafanikio mema katika eneo hili la uchumba, ili uweze kuingia kwenye ndoa na mke/mume aliye sahihi kwako.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com
+255759808081.