Upo wakati ambao mtu anakuwa anautumikia, yaani upo wakati ambao mtu anakuwa anavuna matunda ya matendo yake maovu aliyofanya huko nyuma.
Huenda kwa sasa hana hiyo tabia ila matokeo ya dhambi aliyofanya huko nyuma yanaweza kuonekana sasa. Baada ya kuamua kumrudia Mungu, bado yale matunda ya matendo yake bado yanamfuata.
Wakati mtu huyo anaendelea kuvuna alichokipanda, anapaswa kuwa mvumilivu sana sana. Maana ni kipindi cha mpito, kipindi cha kuchekwa sana na watu, kipindi cha kudhihakiwa na watu wengi wanaomwambia Mungu wako yupo wapi.
Kipindi kama hichi hupaswi kurudi nyuma, haijalishi ulitenda sana mabaya, kama sasa umeamua kumrudia Mungu. Na umeshaomba toba mbele za Mungu, hupaswi kuwa na mashaka.
Unapita katika moto mkali kweli ila isikuvunje moyo wako, endelea kujibidiisha kwa mambo ya Mungu, kuwa mtu wa ibada, kuwa mtu wa kusoma Neno la Mungu, na kuwa mtu wa maombi.
Taratibu utaanza kuona mabadiliko ndani yako, utaanza kuona Mungu akianza kukuinua hatua kwa hatua. Ile aibu yako utaona ikiondolewa kwako, yale magumu uliyokuwa unapitia utaona Mungu akikuondolea na kukufanya ushuhuda mbele za watu.
Neno la Mungu linatutia sana moyo, hasa kama kuna mambo ulimkosea Mungu wako, na sasa umeamua kumrudia Mungu wako. Unapaswa kuvumilia kwa kipindi chote.
Rejea: Nitaivumilia ghadhabu ya BWANA, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea teto langu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake. Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi BWANA, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu. MIK. 7:9-10 SUV.
Usiogope, endelea kumtumaini Mungu, ile aibu yako yote haitakuwepo tena. Wale wote waliosema wa kuokoka atakuwa wewe, aibu yote itawarudia wao.
Umeokoka? Usiogope, endelea na Bwana, hata kama kuna mambo unaona yanakusonga, hata kama kuna mabakibaki ya kwenye dhambi uliyokuwa unaifanya huko nyuma. Bado yanakufuata, Mungu atakuondolea na hayo yote ukiendelea kuwa mwaminifu mbele zake.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.