“Mimi nasema hivi, Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu. Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lo lote limpendezalo. Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini?” Mhu 8:2-4 SUV.
Hadi mtu kuitwa mume au mke, kunakuwepo na mchakato ambao mtu huyo ameupitia hadi kufikia hiyo hatua, kutokana na taratibu za jamii husika au dini husika anayoamini huyo mtu.
Wakristo wana taratibu zao ya kufungisha ndoa, hata kama mtu atachukua bila kufuata taratibu za kikanisa, atakuwa amekosea ila kifamilia itamlazimu afuate taratibu zao zinavyomtaka, kama walichukuana kienyeji kuna adhabu/faini wanaume huwa wanapigwa kwa baadhi ya makabila.
Tukija katika upande wa kanisa, wale wanaotengeneza mambo yao na kuamua kuanza maisha katika Bwana, ndoa zao huwa zinabarikiwa kanisani na Mchungaji au Askofu wao kutokana na taratibu za kanisa husika.
Kuna wale wanaofuata taratibu zote za kifamilia na kikanisa kabla ya kuanza maisha ya ndoa, hupewa Baraka za wazazi na kikanisa, ndoa yao huwekwa mikononi mwa Mungu mwanzoni kabisa mwa maisha yao mapya.
Vipo viapo na makubaliano ambayo huongozwa na kiongozi wao wa dini kuvisema na kuvikubali mbele za watu au mashahidi wengi, wazazi au walezi wa pande zote mbili hutamtaka maneno ya nasaha kwa wawili hawa wanaoenda kuanza maisha mapya.
Viapo wanavyoviapa madhabahuni huwa vina maana kubwa, Mungu anaviheshimu hivyo viapo na makubaliano yaliyowekwa siku wanafungiwa au wanabarikiwa ndoa yao.
Katika maandiko ya biblia niliyoanza nayo hapo juu, mfalme aliwakilisha serikali ya kibinadamu ambayo imewekwa na Mungu. Viongozi wa serikali wanazozifuata sheria za Mungu za maisha wanahimiza kuishi maisha ya haki bila kuoneana.
Mungu anatutaka kuwatii viongozi hawa wanaotuongoza, sasa tunao viongozi wetu wa kiroho ambao ni wachungaji wetu, ambao hutusimamia mambo mbalimbali ikiwemo suala hili la ndoa.
Inapotokea shida yeyote ile kwa wanandoa, wakafikia hatua ya kutengana, wanapaswa kurudi kanisani kueleza yaliyowapata, watapata ushauri kutoka kwa viongozi wao, mambo yakishindikana kuna ushauri wapewa.
Sasa wapo huwepewa ushauri na wengine hujichukulia maamuzi yao wenyewe, sasa leo tuzungumze na mtu ambaye amekutana na changamoto kwenye ndoa yake na hataki kuendelea kuishi na mume/mke wake.
Vitu 3 vya kuzitangatia unapokutana na shida hii;
- Usifanye haraka kumwacha
Ukifanyiwa jambo baya na mume wako au mke wako hasa ukibaini anatembea na mwanaume au mwanamke mwingine, unaweza kuona haina haja kuendelea naye.
Uzinzi kwa wanandoa ni jambo baya na linaweza kuvunja ndoa, lakini unapaswa kuwa makini sana, hadi pale utakapoona ni tabia endelevu na habadiliki, hapo utaweza kuchukua maamuzi.
Ukikimbilia kuachana na ukaona bora uanze maisha na mwanamke au mwanaume mwingine, wahenga wana msemo wao “usiruke maji ukaenda kukanyaga tope” nikiwa na maana kuwa unaweza kumwacha mwenye afadhali ukaenda kukutana na mwenye shida Zaidi.
Hupaswi kuwa na maamuzi ya haraka, unapaswa kutulia kwa muda wa kutosha, hata kama mmetengana, yaani mke wako ameenda kwao au umerudi kwenu au umetafuta sehemu nyingine ya kuishi nje na nyumba yako. Hakikisha unasikiliza ushauri sahihi unaopewa na viongozi wako wa kiroho.
- Usifanye haraka kuoa/kuolewa
Kama kuna eneo wanandoa wengi walioachana huharibu ni hili, wengi hukimbilia kuoa au kuolewa, hasa wanaume kwa kuwa ni rahisi kupata mwanamke mwingine, huoa wangali bado sintofahamu ni kubwa katika ndoa yao.
Hupaswi kufanya hivyo, vizuri ukatulia na kusubiri hali ya hewa itulie, unaweza kufikiri ukioa au ukiolewa haraka utapata tulizo la moyo, unaweza kukutana na tabu nyingine kubwa na itakufanya uchukue uamuzi mbaya.
Nilikuwa na ongea na ndugu mmoja mwanaume, naye alipata shida kwenye ndoa yake ya kwanza akawa ameoa mwanamke mwingine, baada ya kuoa, yule aliyemwacha alimwambia kabisa hakupenda hicho kitu maana alikuwa anataka waendelee kuishi pamoja. Baadaye ndugu huyu alianza kujuta kwanini alifanya maamuzi ya haraka ya kutengana na mwanamke wa kwanza, aliona aliyemwacha alikuwa mzuri.
Nakusisitiza usifanye maamuzi ya haraka ya kuoa/kuolewa, unaweza kupata washauri wabaya wakakuambia haina shida, nakuambia utajutia maamuzi yako, maana huenda hasira na uchungu vilikuongoza kuingia kwenye mahusiano yasiyo sahihi.
Hakikisha unashirikiana na viongozi wako wa kiroho, watakusaidia sana kwenye maeneo mengi, wakiona pagumu kuendelea kuishi na mwenzi wako kutokana na sababu unazowaambia na wanazoziona wao, watakuambia.
- Kuwa na kipindi cha ukimya na utulivu
Unapokutana na shida vizuri kuwa na utulivu wa hali ya juu, mambo mengi yataongelewa juu yako, yapo mazuri na mengine mabaya, hasa mabaya yatakuwa mengi sana. Unapaswa kuwa na ukimya na utulivu wa hali ya juu sana.
Inaweza kuwa ngumu kuwa kimya na mtulivu ila kwa msaada wa Mungu utaweza, unapaswa kumwomba Mungu sana, usiache ibada, usiache kusoma neno la Mungu, haya yanaweza yakawa ni mambo magumu kwako ila unapaswa kujiwekea nidhamu ya kuyafanya.
Ukifanikiwa kustahimili kipindi hichi kwa kukaa kimya na kutulia, utakuwa umejiponya na mambo mengi sana katika maisha yako, kwa sababu nia ya shetani huwa tuharibikiwe Zaidi inapotokea hii shida ya mahusiano.
Baada ya kuzingatia na kuvuka hatua hizi tatu, utapata mwafaka wa jambo lako kwa njia salama kabisa, mwafaka ambao hautakupa aibu na fedheha mbele ya jamii na kanisa lako. Utakuwa salama maeneo mengi sana.
Kumbuka hayo ni maisha yako, chochote utakachofanya kwa kufanya maamuzi ya hovyo, mtu wa kwanza kumuumiza ni wewe mwenyewe na wa pili ni ndugu zako na marafiki zako wanaokupenda.
Mungu atusaidie sana
Samson Ernest
+255759808081