Haleluya, wakati mwingine tena mzuri wa kushirikishana TAFAKARI zetu kwa kile tulichokivuna katika sura ya leo.

Napenda uanze kutazama mambo kwa sura ya viwango, na si kwa sura ya kawaida kawaida. Ukitaka kujenga nyumba yako, hebu fikiri katika viwango vya juu kujenga nyumba nzuri, na si kinyumba cha kinyonge.

Ukitaka kuwa mfanyabiashara wa kimataifa, hebu anza kuwaza biashara yako kimataifa na si ki mkoa. Hata kama umeanza na moja, we ona ukubwa wa biashara yako katika viwango fulani vikubwa.

Ukitaka kuwa na ndoa vya kiwango kizuri cha kiMungu, anza kufikiri kiviwango ambavyo wewe mwenyewe unavyo. Kama huna anza kuvitafuta sasa, kama njia zako zilikuwa za kona kona, anza kuziweka sawa uendane na viwango vya mume/mke unayemtaka.

Kila jambo unalotamani liwe katika viwango fulani, anza kuliishi sasa, usikae bila kufanya ukitegemea utaibuka tu kama uyoga. Uyoga wenyewe una msimu wake wa kuota.

Unafanya/unatoa huduma ya kiroho, tamani huduma yako iwe katika viwango vya kiMungu, huku ukiendelea kumtafuta Mungu kwa bidii. Sio unatamani viwango vya kiMungu umekaa bila kujishughulisha na kile Mungu amekuitia.

Mungu wetu ni wa viwango, unapofanya vitu kinyonge hata yeye anakushangaa mno. Lazima uwe na maono ya mbali, ambayo hata kama wewe hutakula sana matunda yake, wengine watakula.

Mungu anapendezwa sana na hili, tunapomwazia mambo mema ya kumtumikia kwa viwango. Haijalishi tupo kwenye hali gani sasa, tunapaswa kuwaza mambo makubwa ya kumletea Bwana utukufu huko mbeleni, jinsi Mungu anavyozidi kutupa uzima.

Hata kama sasa hivi unauza ubuyu wa shilingi 100, jione wewe ni mfanyabiashara mkubwa wa baadaye. Unapowaza katika viwango vya juu hutouza ubuyu kama muuza ubuyu wa kawaida, utauza ubuyu kama mfanyabiashara mkubwa. Hata hudumia yako ya wateja itakuwa ya viwango vya juu maana ndani yako kuna kitu.

Una huduma yako lakini umeanza kwa chini sana, fikiri kama mtu aliye na huduma kubwa hapo mbeleni. Kuona hivyo hutomtumikia Mungu kwa mazoea mazoea, lazima utakuwa wa tofauti kabisa.

Utasema mtumishi unasema nini mbona sikuelewi, hili tunalithitibisha kwa mfalme Suleiman. Mfalme aliyemjengea Bwana wake nyumba ya kiwango, akaweka vito vya thamani kubwa.

REJEA: na maua, na taa, na makoleo, ya dhahabu, ndiyo dhahabu bora; na mikasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu iliyosafika; na kwa habari za mahali pa kuingia nyumbani, milango yake ya ndani ya patakatifu pa patakatifu, na milango ya nyumba, yaani ya hekalu, ilikuwa ya dhahabu. 2 NYA. 4:21‭-‬22 SUV.

Kwanini mimi na wewe tuwe na mawazo ya kinyonge, kwanini tuwaze kufanya biashara zetu kama watu wasio na matumaini ya kukua kimtaji. Kwanini tufanye kazi ya Mungu kidhaifu kama watu wasio na matumaini ya kuinuliwa zaidi ilivyo leo.

Lazima tumtukie Mungu kwa viwango anavyotaka yeye, lazima tumjengee Mungu nyumba za kweli, zenye kumaanisha kweli tumeiva KIROHO.

Mioyo yetu lazima iwe na kuta za thamani kweli ndani yetu, kuta za NENO la MUNGU ambapo adui akija akute kizuizi kikali.

Chochote unachofanya sasa, hebu anza kukifikiri kiviwango cha juu, usitake vya kinyonge. Nimekwambia hata kama hujafikia hivyo viwango sasa, hilo lisikuzuie wewe kuwa na mawazo ya kiwango.

Hakuna madhara yeyote utakayopata kwa wewe kuwaza kujenga kanisa la watu 10,000, wakati wewe huna hata mshirika mmoja. Hilo lisikuzuie wewe kuwaza mambo mazuri ya KiMungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.