Mliovyoanza kuimba kwa mara ya kwanza na kabla humjawa watu maarufu, mlituvalia nguo nzuri. Lakini Mungu alivyowainua, mkaanza kujulikana na kuwa watu maarufu, mmeanza kutuvalia nguo za ajabu ajabu.

Sasa hivi hamwambiliki, mmeona ngozi zenu za awali ni chafu. Mmeamua kutafuta mikorogo ili mwe weupe.

Uzinzi/uashereti umekuwa kitu cha kawaida kwenu. Mnatumia umaarufu wenu kufanya vitu visivyofaa.

Mmeacha kuogopa madhabahu ya Bwana, mnasimama pasipo wasiwasi huku nyuma mkifanya yasiyofaa mbele za Mungu.

Mkiguswa mnahama makanisa, watumishi wenu wanaogopa kuwaambia maana mnaleta fungu nono la pesa.

Nidhamu ya uchezaji mbele za Mungu imepungua, hakuna tofauti tena ya mtu wa asiyemjua Mungu wala mlango wa kanisa, kuweza kujua huyu ni mkristo na huyu si mkristo.

Nani atawakemea, ikiwa wanaowalea mmewakamata kwa namna mnayoijua wenyewe.

Ni nani atawaonya, ikiwa mnatumia umaarufu wenu kuwavuta washirika wapya wanaopenda kusikiliza nyimbo zenu. Mvuto huu mmewafanya watumishi wakose ujasiri na washindwe kutamka kitu juu yenu.

Nawaonya katika Jina La Yesu, acheni dhambi mrudieni Mungu, vaeni nguo zenye maadili.

Hizi nguo zenu ndio zimewaharibu vijana wengi, leo mdada nguo ambayo akisimama mbele mchungaji anashika kichwa na kushusha macho chini. Ila hana uwezo wa kumwambia acha hii, ndio zimekuwa fashion kwa waimbaji wanaochipukia makanisani.

Tumieni vipaji vyenu vizuri kupeleka watu mbinguni, tumieni umaarufu wenu kuwavuta wengine kwa Yesu.

Mungu haangalii uliimbaje, kama unafanya upuuzi acha mara moja, maana kuendelea kufanya/kutenda hayo hutaiona mbingu, na jehanamu itakuhusu.

Nimeyaandika haya ili ubadilike na umrudie Bwana kwa matendo mema, uamzi unao mwenyewe.

Imeandaliwa na Samson Ernest.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com
+255759808081.