Ukweli kabisa zipo shida zinatupata tukiwa kama wanadamu, shida hizo wakati mwingine huonekana hazina kabisa ufumbuzi wake. Shida hizo zinakuwa hazina majibu kabisa ya kuweza kuzitatua, hata wataalamu wanapokutazama wanaona hakuna kichowezekana kabisa.

Kutowezekana huko kunaweza kutokana na tatizo ulilonalo kuwa kubwa zaidi ya uwezo wao. Pia inawezekana shida uliyonayo hujulikana haina tiba kabisa, tuseme leo UKIMWI umekuwa unajulikana kwa kila mtu kuwa hauna dawa duniani kote kumaliza kabisa hilo tatizo.

Ugonjwa ulionao, inawezekana umezunguka hospitali zote duniani, umepewa majibu ambayo hukuyapenda sana kuyasikia. Ila umejikuta unakubaliana nayo kutokana na uhalisia wenyewe wa tatizo ulilonalo.

Yapo mambo kibinadamu hayawezekani kabisa, hata kama utajiaminisha kuwa utayaweza. Bila msaada wa Mungu hutoweza chochote katika hayo yaliyoshindikana kwa akili za kibinadamu.

Shida uliyonayo kushindikana kwenye hospital kubwa zinazoaminika, haimanishi kabisa tatizo lako haliwezi kupona. Ndio hupaswi kuwa na shaka kabisa ukiwa kama mtoto wa Mungu, sifanyi utani, na wala sina utani wowote na wewe.

Huenda hapo ulipo madaktari wamekuambia hutozaa tena, kutokana na tatizo fulani ulilonalo. Lakini kwa Mungu ni tofauti kabisa na taarifa ya madaktari, utasema mtumishi hayo ni maneno ya kunifariji tu. Unaweza ukawa Sawa kwa jinsi vile unatazama mambo kibinadamu, hebu geuza mtazamo wako hasi, mwamini Yesu Kristo leo.

Hili tunaliona katika maandiko matakatifu, mfalme Nebukadreza baada ya kuota ndoto iliyomfedhesha moyo wake. Alafu hiyo ndoto akawa haikumbuki, aliwaita waganga wote, na waaguzi mbalimbali, walishindwa kumwambia maana ya hiyo ndoto.

Wakaldayo wakawa wawazi kwa mfalme, kuwa hiyo ndoto hakuna anayeweza kuionyesha wazi. Isipokuwa kwa miungu isiyofanya kikao pamoja na wenye mwili.

Rejea: Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionyesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala liwali, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo. Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonyesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili. DAN. 2:10‭-‬11 SUV.

Tunasoma maandiko matakatifu, hakuna mchawi wala mganga aliyeweza kufunua wazi hiyo ndoto. Isipokuwa mtumishi wa Mungu Daniel ndio aliweza kuijua ndoto aliyoota mfalme Nebukadreza na kumpa maana yake.

Rejea: Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni. Danieli akajibu, akasema, Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake. Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa; yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake. DAN. 2:19‭-‬22 SUV.

Mungu anaweza mambo yote ndugu, sijui una shida gani ambayo ulimwengu mzima umesema haitowezekana. Yupo Mungu wa kuwezekana kwa mambo magumu yaliyoshindikana kwa akili za kibinadamu.

Rejea: Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu; lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi; DAN. 2:27‭-‬28 SUV.

Sijui unakabiliwa na nini hapo ulipo, kupitia maneno haya yenye uhai wa pumzi ya Mungu. Amini shida yako ina majibu mbele za Mungu, usimwache Yesu Kristo kwa mazingira yeyote yale.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081