Kama kuna vitu vizuri vya kujifunza katika maisha yetu ya kiroho na kimwili, tunapaswa kujifunza kwa Yesu Kristo mwenyewe, yapo mengi sana mazuri ya kujifunza kwake.

Ukitaka kuongea vizuri, kwa Yesu Kristo ipi elimu ya kutosha namna ya kuongea na mtu/watu, elimu hiyo utaipata kupitia Neno lake.

Ukitaka kufanya huduma iliyo bora ya utumishi na yenye viwango vya juu, unapaswa kujifunza kupitia Yesu Kristo, ambapo utapata elimu hiyo kupitia Neno lake.

Wakati mwingine watu wanalalamika tumewajibu vibaya, kumbe sio kana kwamba wamejibiwa vibaya, ni kwa sababu swali walilouliza kwetu wamepewa majibu yanayoendana na swali lao.

Wapo watu wanakuuliza swali huku tayari wameandaa majibu yao, ukiwajibu nje na majibu yao, wanakuona mtu mbaya kwao, wanakuona una dharau, wanakuona hufai.

Kuonekana hatufai, bado hakuwezi kutuondolea utakatifu wetu, bado hakuwezi kutufanya tuonekane watu wasiomjua Kristo sawasawa.

Yesu Kristo ni mfano wetu hai wa kujifunza kwake, kuna watu wanatuchokoza kwa maneno ya kejeli, wakitaka tuwajibu wanavyotaka wao, tukiwapa majibu yanayostahili wanatuona tuna jeuri, wanatuona hatujaokoka.

Wanafikiri kuokoka kunamfanya mtu ajibu watakavyo wao, hata kama majibu sio sahihi, wao wanataka wajibiwe hivyo hivyo wapate kukufunga kwa kinywa chako.

Rejea: Wakasema wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye.LK. 22:70 SUV.

Kwa kawaida hapo Yesu Kristo alipaswa kujibu ndio kutokana na swali aliloulizwa, lakini hakujibu watakavyo wao, alijibu ‘ninyi mwasema kwamba mimi ndiye’.

Kama msomaji mzuri na makini wa Neno la Mungu, majibu kama haya, Yesu Kristo amejibu sehemu kadhaa pale alipoulizwa maswali yanayofanana kama haya.

Tunaweza kukutana na haya pale watu wanapotushtaki, wanaweza kukuuliza swali la kipuuzi tu kuonyesha dharau, hata kama wanajua kabisa wewe ni mtu fulani unayemtumikia Mungu kwenye eneo fulani.

Ndio maana Biblia inatuasa wakati mwingine mtu anapaswa kujibiwa sawasawa na upumbavu wake, na sehemu nyingine inatupa elimu ya kwamba hatupaswi kumjibu mtu sawasawa na upumbavu wake.

Kwahiyo ukiwa kama mkristo ambaye una Neno la Mungu ndani yako, huhitaji kupangiwa cha kujibu, ikiwa unajua unachojibu hakimkosei Mungu wako, na ukiwa unajua unachojibu unasukumwa na Roho Mtakatifu ndani yako kujibu hivyo. Jibu kwa ujasiri mkubwa bila kumwogopa mtu yeyote.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com