Unajua unapopita katika wakati mgumu huwa kuna akiba ya imani yako mbele za Mungu inabaki hata kidogo. Ila pamoja na kubaki imani yako mbele za Mungu bado kuna watu watakuona umepotea njia kufikiri unavyofikiri wewe juu ya Mungu.
Ukisikia majaribu makali ndio nyakati ambazo hata marafiki zako uliotegemea wana uelewa mzuri mbele za Mungu. Na Roho Mtakatifu yumo ndani yao, ndio wakati ambao watakuchukulia tofauti na jinsi wewe unavyojiona wakati unapita katika jaribu.
Kuna majaribu mengine ni magumu kiasi kwamba unashindwa kuelewa kwanini iwe hivyo, maana ni wakati ambao Mungu mwenyewe anakuwa kimya kwako, hasemi chochote na wewe.
Tunajifunza kwa Ayubu anakutana na mapigo ambayo mengine yanaendelea kuletwa na marafiki zake, wanaona Ayubu haelewi anachokisema, wanamwona ametenda dhambi. Lakini Ayubu mwenyewe hajui amekosea wapi na bado anakiri ukuu wa Mungu kwake, anaelewa Mungu ni mkuu siku zote.
Anakuja rafiki yake mmoja aitwaye Sofari, anampa maneno makali makali kama ni kuua kabisa imani yake. Basi ndio ilikuwa kipindi hiki maana hataki kabisa kuamini Ayubu hajamtenda Mungu dhambi.
Kwa wewe ambaye hujui, Sofari ni mmoja wa marafiki zake Ayubu waliokuwa wapo karibu naye sana katika mapito yake magumu. Walimwona mateso anayopitia ni mateso ya mtu aliyemtenda Mungu dhambi.
Hebu fikiri tumenena mangapi juu ya watu waliopatwa na shida, tukifikiri wamemtenda Mungu dhambi. Kumbe shetani anaweza kutumia wale wale ambao wanaonekana wamesimama na Yesu, kuwaumiza wengine wanaopitia magumu.
Sofari angejua anatumiwa na shetani kumgandamiza Ayubu angenyamaza kimya, kumbe NENO hili hili la Mungu linaweza kutumiwa na shetani kukulaghai mtu wa Mungu.
Unajua ni mambo mazito kabisa, Neno la Mungu kutumika kinyume na mpango wa Mungu. Unaweza kusema unajua sana maandiko ikiwa huna Roho Mtakatifu ndani yako nakwambia utatadanganywa tu.
Hebu fikiri Sofari anamwambia Ayubu hizi habari, usije ukasema alikuwa anampotosha Ayubu, alikuwa anampa uhalisia wa Mungu ulivyo. Kama ni mtu aliyekuwa anamjua Mungu nusu nusu hapa ndio ilikuwa saa yake ya kumsokesea Mungu wake, kabisa Nakwambia.
Rejea; Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi? Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe? Cheo chake ni kirefu kuliko dunia, Ni kipana zaidi ya bahari. Yeye akipita, na kufunga watu, Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia? Kwani yeye awajua watu baradhuli; Huona na uovu pia, hata asipoufikiri.AYU. 11:7-11 SUV.
Napenda uone safari yako ya wokovu kwa sura ya tofauti kabisa, unaona hoja anayopewa hapo Ayubu. Yaani kama ni kubadilisha yale mawazo ya kumwamini Mungu ni kama hivi unavyoletewa maneno mazito kiasi hiki.
Kwa kawaida huyu Sofari alikuwa na sababu ya kumfariji huyu Ayubu, ila wasiwasi wake ulikuwa unamwona amemkosea Mungu. Bila kujua Sofari mawazo aliyonayo juu ya Ayubu mkono wa shetani unahusika kwake.
Tunapata somo kubwa tunapaswa kusimama na Mungu wetu kwa miguu yetu wenyewe bila kusimamia ya wengine. Maana hapa Ayubu hajui kama Mungu anajivunia kwake ndio maana amekaa kimya bila kumwambia jaribu analopitia yeye ndio ametoa kibali.
Huenda Ayubu angejua Mungu ameruhusu hayo au angesikia sauti ya Mungu inayomwambia yeye ndio amesababisha hayo. Nina uhakika Ayubu angekuwa na ujasiri mkubwa zaidi mbele za watu, ila ujasiri wake ulibaki tu kwa jinsi anavyomwelewa Mungu wake.
Mjue sana Mungu ili usimtende dhambi, hata kama itafika muda atakaa kimya juu ya shida yako. Bado utaendelea kulitukuza jina lake kwa matendo yake makuu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.