Kuonekana huna haki ya kupata mgao wa mali za nyumbani kwenu, sio jambo geni kwenye masikio yetu na macho yetu.

Tumeona watu wakifanyiwa hayo, na wengine ni ndugu zetu kabisa tumeona wakitokewa na hayo.

Wengine hatujashuhudia au hatujasikia kutoka kwa watu tunaowafahamu au tusiowafahamu.

Wengine yametutokea sisi wenyewe, kwenye familia zetu, kwenye kazi zetu.

Imefika mahali unafukuzwa kama mtu asiyehusika na mali hizo.

Lakini tunajifunza kwa Yeftha alitengwa na ndugu zake kutokana na kuzaliwa na mwanamke kahaba.

Kwa lugha rahisi na ya kueleweka ni kwamba ni wale watoto wanaozaliwa nje ya ndoa. Kwa hiyo Yeftha alikuwa mtoto wa mama mwingine.

Sifa kuu ya Yeftha alikuwa mtu hodari, mtu mwenye uwezo wa kupigana vita.

Walivyomfukuza, baadaye walikuja kumbuka pale walipozidiwa na maadui zao.

Rejea: Wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu?AMU. 11:6‭-‬7 SUV.

Wapo watu wanaweza kukuona hustahili kwao kutokana na maslahi yao binafsi.

Ukweli ni kwamba kama utasimama na Mungu wako vizuri, uwe na uhakika watakukumbuka tena na kuhitaji msaada wako tena.

Hili tumejifunza kutoka kwa Yeftha, ni mfano hai wa kutusaidia kusonga mbele zaidi.

Hata pale tunapojikuta tupo mazingira ya kukataliwa na ndugu zetu, tuendelee kumwamini Mungu wetu.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
Mtenda kazi katika shamba la Bwana.