Kazi njema itabaki kuwa njema tu, hata kama inaonekana ina idadi ndogo ya watu wanaonyesha wazi kuikubali hiyo kazi, lakini katika uhalisia usioonekana kwa haraka kwa haya macho ya nyama. Wengi sana watakuwa wanaikubali kazi unayoifanya, hata kama hawakuambii na kukupongeza kwa uwazi kwa kazi njema.

Unaweza kufika mahali ukajisikia vibaya na hali ya kukata tamaa ikakuvamia/ikakuvaa ndani yako, ukifikiri hakuna watu wanaojali kile unafanya, kile unatumia nguvu kubwa kufanya, kile unatumia muda wako mwingi kufanya.

Wakati mwingine badala ya kupokea shukrani, unapokea kejeli au dharau nyingi za watu wakionyesha kukerwa na kazi yako au huduma yako nzuri.

Unaweza ukawa ulikuwa mchapa kazi mzuri sana kazini kwako, lakini cha kushangaza kwako na huamini mpaka sasa, hujawahi kupongezwa kwa uwazi kwa kazi nzuri unayoifanya. Mambo mengi yanafichwafichwa, japo utendaji wako wa kazi wanaukubali sana na wakati mwingine wanakujadili kwenye vikao vyao.

Wanakujadili kwenye vikao vyao, lakini hakuna mwenye ujasiri wa kuja kukupa maneno ya kukutia moyo kwa bidii yako kazini, kwa bidii yako kwenye huduma, kwa bidii yako kwenye masomo, kwa bidii yako ya kuwajali wengine.

Unapojikuta upo kwenye hali kama hii, usije ukaacha bidii zako za kufanya mambo yako kwa ufanisi mkubwa, usichokijua ni kwamba wanakukubali sana. Ila hawawezi kuonyesha kwa uwazi kuwa wanakukubali, kwa sababu wanajua ukionyesha kwa uwazi hawana kazi.

Wapo watu wanatetea maslahi yao, unapokuwa hukubaliki na wakubwa, alafu akaonekane mtu yeyote kuonyesha kukubali kwa kazi zako. Huyo mtu atakuwa haipendi kazi yake au atakuwa haipendi nafasi yake yake aliyowekwa na wakuu. Ndio wengi huwa wanakaa kimya.

Tunajifunza kwa Yesu Kristo, wapo watu wengi sana walimwamini Yesu Kristo kwa mambo mbalimbali aliyoyadhihirisha kwao. Lakini changamoto iliyokuwa inawakabili ni pale walipoogopa kutengwa na sinagogi.

Rejea: Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. YN. 12:42 SUV.

Kupitia andiko hili, nikwambie kwamba, kama jambo unalolitenda linamletea Mungu wako sifa na utukufu, alafu hilo jambo likawa haliungwi mkono na watu wengi. Usije ukafika mahali ukavunjika moyo na kuamua kuacha kile ulichokuwa unafanya.

Ipo idadi kubwa sana ya watu wanaokuelewa na haipiti siku bila kukufuatilia ulichofanya au unachofanya au ulichotoa. Siku ukiwaona wote waliokuwa wanakufuatilia na kukubali, utashangaa vile walivyo wengi sana.

Usikubali kuvunjwa moyo na idadi ndogo ya watu wanaoonyesha kukuamini na kukufuatilia kwa karibu kwa kile unafanya. Idadi hiyo ndogo ni picha tu ya watu wengi waliopo nyuma yako.

Zingatia sana katika huduma yako unayotoa, usije ukakubali kurudishwa nyuma kirahisi. Songa mbele bila kujalisha uchache wa wanaokuunga mkono.

Umehubiri zako habari za Yesu Kristo, alafu unaona hakuna anayekuja kuokoka, hilo lisikufanye ujione hukufanya chochote. Watu wamekuelewa sana, sema wengi wao wanaogopa waume zao, wapo wanaogopa wazazi wao, wapo wanaogopa ndugu zao, na wapo wanaogopa marafiki zao.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com