“Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni”, Lk 22:33 SUV.

Petro alikuwa ni mmoja wa wanafunzi wa Yesu mahiri na waliokuwa karibu sana na yeye, ukimfuatilia Petro utaona matukio kadhaa aliyoyafanya akiwa na Yesu, huyu huyu Petro ndiye aliyeahidiwa baadhi ya ahadi na Yesu.

Urafiki wa Petro na Yesu ulikuwa mkubwa sana, tunaona Petro alifika mahali akamkata mtu sikio, wakati ambao Yesu alikuwa akisumbuliwa nay eye hakupenda hilo.

Alifika mahali akamhakikishia Yesu watakuwa pamoja naye popote, ikiwa ni gerezeni ataenda naye, ikiwa ni kifo atakufa naye, kauli hizi zinaonyesha urafiki ulioshibana haswa.

Hakuwa anatania wakati anamwahidi Yesu hayo yote, alikuwa anaongea kwa kumaanisha pasipo kujua alichokuwa anakiongea kinaweza kisiwe vile aliahidi.

Yesu alimuweka wazi Petro kuwa jogoo hatawika atakuwa amemkana mara tatu, Yesu alikuwa na uwezo wa kuona mambo ya kesho au anayoyawaza mtu ndani ya mawazo yake.

“Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui”, Lk 22:34 SUV.

Kulivyoanza misukosuko ya mateso ya Yesu, Petro alikuwa na Yesu, inaonyesha wazi ujasiri wa Petro ulianza kupungua kutokana na matisho mbalimbali aliyoyashuhudia Yesu akiyapitia.

Baada ya Yesu kukamatwa mjakazi mmoja alianzisha kumbainisha Petro kuwa alimwona akiwa na Yesu, bila kuchelewesha alikana kabisa kuhusishwa na hilo, baada ya muda kupita mtu mwingine alimtaja, aliendelea kukana, na mtu wa mwisho alivyomtaja alimkana vilevile.

“Na walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro akaketi kati yao. Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika”, Lk 22:55-60 SUV.

Tunajifunza nini kupitia mkasa huu, tunao marafiki zetu wa karibu sana, watu ambao tunashirikiana nao kwa mambo mbalimbali katika maisha ya kila siku. Ambapo umefika mahali unaona kabisa hata itokee nini watakuwa pamoja na wewe, vile unajitoa kwao na mnavyoshirikiana nao.

Nataka nikueleze ukweli huu, acha kuweka asilimia zote kwa mwanadamu mwenzako, upo wakati atakukataa, sio kana kwamba hawakupendi, shida iliyokupata itakuwa imewatisha na hawatakuwa tayari kuingia kwenye hiyo shida.

Shida zingine zinasababisha hata wazazi wetu watukimbie, wakati ambao utajiona mpweke, wakati ambao unaweza kulaani kila mtu unayemjua alikuwa wa karibu yako, bado haitasaidia chochote.

Kumbuka sisi ni binadamu, huwa hatupendi kupoteza maisha yetu kwa jambo ambalo unaona unaweza kuepukana nalo, utasema acha apambane mwenyewe, wakati mwingine unaweza kuzungumza maneno ya kumuumiza aliyepatwa na shida. Mfano “atajijua mwenyewe, nani alimwambia afanye hayo, ubishi wake umemponza”.

Sisi kwa asili ni waoga, ubinafsi pia umo ndani yetu, Mungu asipokuwa pamoja nawe utakufa watu wanakuangalia kama hawakujui, utasema hapana sio kweli! Wangapi wametekemea kwa ajali za moto wakilia niokoe na hakuna aliyewasogelea kwa kuogopa kuungua moto.

Narudia tena, mtegemee Mungu wako, huyu ndiye mwenye watu, anaweza kumpa ujasiri yeyote akasimama na wewe, na asipotokea wa kusimama na wewe, yeye bado atakuwa pamoja na wewe hadi unavuka jaribu lako salama.

Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha.
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081