Ukishasema nimeokoka tu, ni kama vile umetangaza chuki baina ya ndugu zako, majirani zako, na marafiki zako. Unaanza kushindwa kuelewa vizuri, wakati hujaokoka haikuwa hivyo kabisa, lakini baada ya kuokoka tu, umeanza kukumbwa na hiyo mikasa.
Dharau zinaweza kuongezeka kwako, hasa unapokuwa na huduma, wataonyesha kila dharau, kuonyesha msisitizo kuwa hutaweza kufika mahali popote. Na usipokuwa makini hapa unaweza kuona wokovu unakuwa mgumu sana kwako, na wakati mwingine unaweza kukosa ujasiri wa kufanya kile Mungu alikuitia.
Miaka ya nyuma sana, huko kijijini kwetu, kulikuwa na ujenzi wa kanisa kubwa sana kwa huko kijijini. Nasema kubwa kwa kijijini maana kwa mjini linaweza kuwa dogo. Walipoanza ujenzi, walianza vizuri, ila walipofika hatua ya madirisha walikwamia hapo. Walikwama kwa muda mrefu kidogo, mtu mmoja akawa anipa habari jinsi watu walivyokuwa wanatoa maneno ya kejeli.
Sasa ikawa walevi wakitoka kulewa huko, ile jioni wakati wanarudi nyumbani, walikuwa wanapigapiga ule ukuta na kusema maneno ya dharau.
Maneno waliyokuwa wanasema ni haya, hawa wakristo wameshindwa, hawataweza kujenga hili kanisa. Ilikuwa ni dharau na kejeli za waziwazi, ukizisikiliza unaweza kukosa ujasiri kabisa badala yake aibu inakuvaa.
Hata katika maisha yako, huenda hapo ulipo una maisha fulani hivi ya chini sana, alafu wakati huo umetangaza kuokoka. Maneno yatakayofuata nyuma yako, yanaweza kuwa mwiba mkali sana kwako.
Unaweza kuanzisha kabiashara chako, kwa kuanza na kamtaji kadogo, ukakutana na maneno makali, sio makali tu, yamejaa dharau ndani yake. Utasikia huyu mlokole naye biashara ameiweza tangu lini, huyu si anajua kuomba tu na kushinda kanisani.
Unaona maneno kama hayo ya dharau, kama usipomsikiliza Mungu vizuri, unaweza kuacha kabisa kile ulinzisha katika maisha yako.
Si hayo tu, unaweza kuwa umekaa muda mrefu sana bila kuolewa, ikatokea kuolewa kwako, utasikia wa kuolewa ndio huyu!! Maneno ambayo ukisikia ni machungu sana kwako.
Inaweza ikawa kwa jinsi ya familia yako ilivyo, watu wanavyojua ulipotokea, labda umeonyesha kukataa hiyo hali ya udhaifu walioishi wazazi wako, ukathubutu kufanya mambo makubwa. Utasikia Maneno mabaya yakiinuka juu yako, unaweza kusikia hadithi kibao zinazokufanya usiendelee na kile ulianza kufanya.
Pamoja na maneno mabaya, pamoja na vizuizi vyote unavyokutana navyo, pamoja na maneno ya dharau, pamoja na maneno ya kukupiga vita ili usiweze kuendelea. Ikiwa umeokoka kweli kweli, na Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wako, fahamu hivyo vita si vyako.
Wote wanaolitii Neno la Kristo, sio kulitii tu, wanapolisikia wanatetemeka, watu wale wapo salama salimini mikononi mwa Mungu.
Rejea: Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi msikiao neno lake mkatetemeka: Ndugu zenu ambao wanawachukia, na kuwapiga marufuku kwa sababu yangu, wamesema kwa dharau Mungu na aoneshe utukufu wake, nasi tuwaone nyinyi mkishinda! Lakini wao wenyewe ndio watakaoaibishwa! Isaya 66:5 BHND.
Wale wanaokutisha, wanaokuambia tutaona Mungu wako yupo wapi, wanaosema kila neno baya juu yako. Uwe na uhakika hao watu Mungu ataenda kuwaibisha siku moja, acha waongee maneno yao yasiyofaa, maana hawajui aliyekuita ndio anajua mwanzo wako na mwisho wako.
Tena Mungu anakazia zaidi, hata ulimwengu mzima ukiwachukia, ujue wanamchukia Mungu, na si wewe!! Sijui kama unaelewa vizuri hili, hebu tusome hili andiko;
Rejea: Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Yohana 15 :18 SUV.
Kama ulifika mahali ukaanza kuona wokovu umekushinda, tubu kwa hilo, wewe upo salama kabisa. Hayo wanayokufanyia wasiomjua Mungu wa kweli, hawakufanyii wewe, wanamfanyia Mungu wako.
Kama ni hivyo, sasa unataka utoke ndani ya wokovu uende wapi? Hakuna pa kwenda, umeshajua vita vinavyoinuka juu yako, hivyo vita si vyako, bali ni vya Bwana.
Mungu akubariki sana.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081