Haleluya,

Unaweza kuteswa sana na jambo ukafikiri anayekuhangaisha ni mtu ambaye hamfamiani kabisa. Muda mwingine unaweza kufikiri hilo jambo linalokuhangaisha unaweza kumshirikisha rafiki yako kwa kumwona anaweza kukusaidia, unakuwa huru kumweleza kile kinakusumbua.

Kumbe unavyomweleza vitu vyako ndio anapata nafasi zaidi ya kuendelea kukukandamiza chini zaidi. Mpaka uje ujue kinachokuangamiza ki nguoni mwako, utakuwaumeumizwa vya kutosha.

Adui zetu hawatoki mbali sana, ni wale wale tunaokula nao, ni wale wale tunaocheka nao, ni wale wale tunaofanya nao kazi ofisi moja, ni wale wale majirani zetu, ni wale wale tunaofanya nao huduma moja ya kiroho.

Wanapokuja kutugeuka mara nyingine huwa tunashindwa kutambua kuwa kinachotusumbua tunacho karibu nacho. Wakati mwingine ukielezwa adui yako ni rafiki yako unaweza kukataa kutokana na ukaribu wenu.

Sikuambii uanze kuogopa watu, sikuambii usiwe na marafiki, sikuambii uanze kuishi ki vyako vyako na sikuambii uache kushirikiana na watu. Maisha hayapo hivyo, unapaswa kujua haya ili uwe makini na ujue haya mambo yanaweza kukutokea wakati wowote.

Unaweza kuwa unakutana na changamoto ngumu kazini kwako, kumbe kuna maneno mabaya anayapelekewa boss wako na rafiki yako wa karibu sana. Unaweza kuhangaika kumtafuta mchawi ni nani, kumbe ni huyo huyo unayemshirikisha mambo yako ya ndani na wakati mwingine kumweleza changamoto zako unazopitia wakati huo.

Unaweza kusema una nini mpaka majirani zako wote wakuchukie, kumbe moja ya ndugu/rafiki zako unaowaamini na kuwashirikisha baadhi ya mambo yako ya ndani. Wanakusambazia maneno mabaya juu yako kwa majirani zako.

Vita vingine havitoki mbali, chunguza vizuri utaelewa zaidi hichi ninachokueleza hapa. Napenda uishi maisha ya kufurahia uwepo wako duniani, nimefurahi zaidi biblia inatufunulia haya ili tuweze kufunguliwa baadhi ya maeneo tuliyofungwa ufahamu wetu.

Rejea: Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. ZAB. 55:12‭-‬13 SUV.

Anayekusumbua sio adui wa mbali, ni rafiki yako wa karibu sana, tena unajuana naye sana sana. Sio mimi nasema ni maandiko matakatifu yanasema hivyo.

Lakini pamoja na hayo yote, jiambie maneno haya;

Rejea: Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? ZAB. 56:11 SUV.

Watahangaika sana juu yako, usiku na mchana, lakini amini hawatakuzuru kwa chochote. Hata kama watakuwa hivi;

Rejea: Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu, Mawazo yao yote ni juu yangu kunitakia mabaya. ZAB. 56:5 SUV.

Hata kama wamepeleka taarifa kwa boss wako kuwa hufai kuwa kiongozi ili wao wachukue nafasi yako, amini hawatafanikiwa ikiwa utaendelea kubaki na Yesu Kristo.

Hata kama watapeleka taarifa mbaya za kutunga, kwa mchumba wako ili mwachane, amini mipango yao haitafanikiwa kama huyo ndiye Mungu amesema ni mume/mke wako, hawataweza kuwatenganisha kamwe.

Hata kama wataenda kupeleka taarifa mbaya kwa mume/mke wako ili uachike au mfarakane, amini mipango yao haitafanikiwa. Haijalishi adui yako unayo miguuni pako, hatafanikiwa kamwe hata kwa hatua ndogo utamwona anaanza kufanikiwa kukuangamiza uwe na imani hatafikia lengo lake kuu.

Mungu akiwa upande wako usiwe na hofu, nenda mbele zake kumtwisha mizigo yako, eleza shida zako zote naye atakusaidia.

Rejea: Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele. ZAB. 55:22 SUV.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.