Upo utata ambao unaweza kujijengea ndani ya fikira zako, ukiwa unafikiri upo sawa kwa hayo unayofikiri. Unaweza kuona watu wengine wanakosea sana wanapotaja jambo unaloona wewe sio sahihi.

Kujua mistari michache ya Biblia, wakati mwingine hutufanya tujione tumejua kila kitu ndani ya biblia. Tunaona hata mtumishi wa Mungu anaposema jambo ambalo sisi hatujui andiko lake lipo wapi, anakuwa anakosea.

Tunapaswa kutoamini kila Neno, hiyo ni kweli, ila hatupaswi kupinga kila Neno, bila kujua maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hilo tunalopinga.

Kujua maandiko matakatifu nusu, kwa kufikiri tumeshajua kila kitu, inaweza kutufanya tukafunga milango ya kujifunza zaidi Neno la Mungu.

Muda mwingine tumeingia kwenye mabishano ya mambo ambayo tunaona siyo sahihi na ni dhambi. Kumbe kutokujua kwetu maandiko matakatifu kunatufanya tuone hivyo, ila sio kweli ni dhambi.

Inaweza isiwe rahisi kujizuia kuingia kwenye mijadala ya mabishano ya mambo tunayoona wengine wanapotosha, na sisi tunakuwa tunaona tuna majibu yake sahihi.

Vyema kuwa na akiba ya maneno, ikiwa huna uhakika na jambo asilimia mia moja, wakati mwingine unaweza kubisha na kuwaona wengine wanatenda dhambi. Kumbe ni muono wako binafsi, ila watu hawatendi dhambi yeyote.

Busara pia kukubali kujifunza jambo unaloona linakupa utata, ikiwa itakuwa ngumu kupata majibu ya moja kwa moja. Vyema kujipa muda zaidi wa kuutafuta ukweli ulio sahihi, kupitia Neno la Mungu.

Kichwa cha somo huenda kimekuvuta kujua zaidi, huenda ulishaanza kunihukumu kutokana na kuujua ukweli. Na huenda umejikuta unasoma hapa, kwa sababu unaniunga mkono kwa jinsi ulivyoona kichwa cha somo.

Kuna kipindi nilikutana na ujumbe wa mtu akiwa anahoji uhalali wa watumishi wa Mungu kusema, Mungu ni mume wa wajane. Binafsi sikuwa na andiko la moja kwa moja linalothibitisha ukweli wa kauli hiyo.

Huenda ningejua andiko ninaloenda kukushirikisha hapa, ningemjibu huyu ndugu kwa ujasiri zaidi. Ila nilijipa subira na uzuri halikutoka moyoni hili jambo, ndio maana leo nimeweza kukumbuka haraka nilivyokutana na hili andiko ninaloenda kukushirikisha hapa.

Hapa ndipo ninapoendelea kuthibitisha kuwa Neno la Mungu ni hazina kubwa, pia nazidi kuelewa kwamba, zipo Elimu nyingi za upotoshaji tunaziamini na kuzishikilia. Tena wakati mwingine sisi wakristo ndio huzitoa hizi Elimu, hii ni kutokana na kutolijua Neno la Mungu vizuri.

Nikukuhakishie kwamba, wanaosema Mungu ni mume wa wajane, hawajakosea kabisa, ndio hawajakosea, na kama ulikuwa umeanza kusita kuhusu hili. Leo utaenda kulithibitisha hili kupitia Neno la Mungu.

Rejea: Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya UJANE wako hutayakumbuka tena. Kwa sababu MUUMBA wako ni MUME WAKO; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. ISA. 54:4‭-‬5 SUV.

Nimejaribu kuwekea kwa herufi kubwa kwa mkazo zaidi, bila kupunguza andiko, wala bila kuongeza chochote. Kama umesoma haraka, nikuombe urudie tena kusoma, lipo jambo la kujifunza hapo.

Siku nyingine usiwe mwepesi wa kukubali jambo kwa sababu umekosa andiko, jipe muda, ikiwa ni msomaji mzuri wa Neno la Mungu. Amini ipo siku hilo linalokutatiza kichwani, litatuliwa na Mungu mwenyewe kupitia Neno lake.

Kama ulishaanza kupata wasiwasi na wanaosema Mungu ni mume wa wajane, fahamu kuanzia leo hawakuwa wakikosea. Bali walikuwa sahihi kabisa, sema wewe ndio ulipata fundisho lisilo sahihi kwako.

Usiache kujifunza Neno la Mungu, maana limebaba hazina kubwa ya maisha yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081