Kuna Mithali moja inasema hivi, sikio la kufa halisikii dawa, na msemo mwingine ukasema bora kumwelimisha MJINGA ataelimika, kuliko MPUMBAVU. Maana mpumbavu ni mtu mjuaji sana anayejiona anajua kila kitu, kumbe hajui chochote. Mpumbavu utabishana nae kuanzia asubuhi mpaka jua linachoea, hamtoelewana kamwe wala hamtofikia hitimisho/mwafaka.
Kwanini nayasema haya, wengi sana wanaambiwa mahali ulipo sio sahihi, badala kusikiliza kile wanaambiwa na kukifanyia uchunguzi kwa njia ya Neno la Mungu na maombi. Wao wanaona watu hawawapendi manabii wao.
Mchungaji wa uongo, mwalimu wa uongo, mwinjilisti wa uongo, mtume wa uongo, na nabii wa uongo. Sio lazima wawe nje ya makanisa mengine, hayo hayo makanisa unayoona yapo sahihi, utakuta shetani amepenyeza wakala wake humo kupotosha watu wa Mungu.
Kwa sababu watu wameshikilia dini zao, kwa sababu watu wameshikilia manabii wao kuliko Mungu. Huwezi kuja kumwambia hapo ulipo sio mahali sahihi akakuelewa kirahisi. Ukijaribu kugusa dhehebu lake uwe na uhakika mtagombana, ukijaribu kumgusa nabii wake uwe na uhakika huo ugomvi utakuwa mbaya sana.
Mwingine atakwambia sitaki umguse baba yangu wa kiroho, huyo baba yake wa kiroho, ndiye anampotosha na kumjaza elimu potofu. Huyo baba yake wa kiroho ndio anayemtabiria ndoto za uongo.
Na manabii wa uongo wana mbwembwe nyingi haijawi tokea, wana majivuno mengi kweli kweli, wanajipaga majina makubwa kweli kweli. Hakuna nabii wa uongo anajishushaga, wote wapo juu, wanajua kucheza na akili za washirika wao kweli kweli.
Huwezi kumkuta mshirika wa nabii wa uongo akiwa dhaifu dhaifu, wote wako imara kweli kweli. Wamelishwa mafundisho potofu kiasi kwamba ukienda kichwa kichwa na hoja zako unatolewa nje.
Kuwepo manabii wa uongo, sio kana kwamba wa ukweli hawapo, manabii wa ukweli wapo, na wanatumia maandiko matakatifu. Hawatumii akili zao wenyewe kutunga nabii za uongo, wala hawaleti ndoto za uongo.
Wapo watu wanampenda kweli Mungu wao, ila wapo mahali pasipo sahihi, mahali ambapo wanalishwa uongo. Wanatabiriwa uongo ambao Mungu hakuwapa hao manabii watabiri, ila kwa kuwa wanaotabiriwa wanaona sawa. Wanazidi kufurahia hayo mambo, bila kujua ni upotovu.
Siandiki mambo ninayoyatunga kichwani, nasema mambo ambayo yapo kimaandiko na tunayaona kwa macho yetu tunapoishi katika mazingira yetu.
Rejea: Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema BWANA, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema BWANA. YER. 23:32 SUV.
Umeona hapo, manabii wa uongo si tu wanatabiria watu uongo wao wakutengeneza, wana majivuno mengi ya kipuuzi. Majivuno ya kujikuza wao tu kuliko Mungu wao.
Mungu akupe ufahamu uweze kuelewa haya.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.