Mpaka sasa wapo watu wanaamini pasipo miungu yao, mambo yao hayawezi kwenda vizuri.

Siku moja nikiwa natoka wilaya moja ya Singida kurudi mjini, nilipata usafiri wa mtu binafsi badala ya gari la abiria.

Ndani ya gari lile aina ya Noah, kulikuwa na pombe ya kienyeji imewekwa ndani ya galoni ya lita 5. Kumbe ile pombe ilishakaa muda mrefu sana, baadaye ikalipuka na kumwagikia baadhi ya watu waliokuwa karibu na hiyo pombe.

Huyu baba ambaye baadaye nilikuja kugundua alikuwa askari, aliomba msamaha kwa wale watu waliomwagikiwa na pombe ile.

Alichosema ni kwamba, Samahani sana, tumetoka kwa wazee kutambika, wakatupa pombe ya kuondoka nayo. Kauli ile ilinifanya nifikiri sana na kujua kumbe wapo watu wanaamini sana miungu yao kuliko Mungu wa kweli.

Kwanini nakueleza haya, huu mfano hai unaendana sana na somo la leo, wapo watu wanaamini pasipo miungu yao, pasipo miungu ya mababu zao. Mambo yao hayawezi kwenda vizuri kabisa, na wakirudi kuiabudu miungu yao wanaamini mambo yao yanaenda vizuri.

Mtu anaweza akawa kanisani kabisa ila akawa mhudhuriaji mzuri wa ibada za miungu ya mababu zao au mababa zao.

Anaamini akishafanya ibada ya miungu ya mababu zake, mambo yake yataenda vizuri sana. Na kweli asipofanya ibada ya miungu ya mababu zake, anaona mambo yake hayawezi kwenda vizuri.

Mtu yule anakuwa anategemea miungu mingine kumsaidia mambo yake, bila kuelewa kitendo kile kinamchukiza sana Mungu aliyemuumba.

Hili tunapata kulijua vizuri kupitia kwa wana wa Israel(Yuda&Yerusalemu) waliona malkia wa mbinguni(mungu mke) ndiye aliyekuwa anawasaidia mambo yao.

Wakati nabii Yeremia anawaletea ujumbe wa Mungu kuhusu kuabudu kwao malkia wa mbinguni(mungu mke) walisema hivi;

Rejea: Lakini tulipoacha kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, tumepungukiwa na vitu vyote; na kuangamizwa kwa upanga, na kwa njaa. Nasi tulipomfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, je! Tulimfanyizia mikate, ili kumwabudu, na kummiminia mamiminiko, waume zetu wasipokuwapo? YER. 44:18‭-‬19 SUV.

Hawa ndugu waliona baada ya kuacha kumwabudu mungu wao, matatizo mengi yaliwapata, kwa hiyo wakawa wanalalamika kuhusu hilo jambo.

Leo wapo watu watakwambia, miungu ya mababu zao ndio inawasaidia mambo yao. Ukimweleza habari za Yesu Kristo anakuona hujui chochote, japokuwa anajiita mkristo.

Hawa wana wa Israel sio kwamba walikuwa hawamjui Mungu wao wa kweli, walikuwa wanamjua vizuri sana ila walifika mahali wakaanza kuabudu mungu mwingine(malkia wa mbinguni).

Mwabudu Mungu wa kweli, achana kabisa na miungu mingine, kuabudu miungu mingine ni chukizo kubwa sana mbele za Mungu.

Mungu akubariki sana.