Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, namrudishia Mungu sifa na utukufu kunipa kibali hichi tena cha kuweza kukushirikisha tafakari hii.
Tunazungukwa na idadi kubwa sana ya watu mbalimbali, wanaomjua Mungu na wasiomjua Mungu. Katika hao wasiomjua Mungu muda mwingi utakuta wanaongea vitu visivyofaa.
Najua umewahi kujenga mashaka na rafiki yako baada ya kumwona yupo na kundi fulani la watu unalolijua lina tabia fulani mbaya. Najua umewahi kujenga mashaka na mtoto wako baada ya kumwona anaambatana na kikundi fulani cha vijana wavuta sigara, na wanywaji wa pombe.
Najua umewahi kuwa na mashaka na mke/mume/mchumba wako, baada ya kumwona ana mahusiano ya karibu sana na watu unaowajua tabia zao ni mbaya. Hapa lazima uanze kupiga kelele maana unajua sumu anayoenda kuachiwa na marafiki wale ni mbaya sana.
Hatukatai kuwa sawa na watu wote, huzuiliwi kuonekana upo na mtu fulani ambaye jamii inamjua sio mtu wa tabia njema. Tunajiuliza kipi kinamvuta mtu yule kwako ambaye tabia zake na zako zinaonekana tofauti, kipi kinampa rafiki yako ujasiri wa kukupa maneno ya ovyo ikiwa anajua wewe ni mtu wa namna fulani unayejiheshimu.
Wakati mwingine hatuwezi kuwakwepa hawa washauri wetu ambao ni marafiki zetu, kwa sababu wakati mwingine tunaishi nao nyumbani. Tena ni watu wetu wa karibu mno na tunaheshimiana nao kama dada, kaka, mama, na baba.
Labda inatokea unakutana na changamoto ya ndoa yako, alafu unakutana na rafiki anakuambia achana na mume/mke wako oa/oelewa na mwingine. Na wewe unakubali, na kusahau Mungu anazuia hilo jambo.
Tunajua andiko linasema tuwaheshimu wazazi wetu ili tupate kuishi siku nyingi, heshima ile haimanishi mzazi wako akikutuma ukafanya jambo baya umtii kwa sababu ni mzazi. Sio ukiambiwa ukaibe na wewe unaenda kuiba kwa sababu mama/baba alikuambia.
Haijalishi ni mzazi wako au mtu unayeheshimiana naye vizuri sana, kama atakupatia ushauri usiofaa. Epukana naye mbali sana kwa kupuuza ushauri wake, ili kuokoa mahusiano yako na Mungu.
Hebu rejea mistari ifuatayo utanielewa zaidi ninachokisema hapa;
*Ahazia alikuwa na umri wa miaka arobaini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri. Yeye naye akaziendea njia za nyumba ya Ahabu; kwa kuwa mamaye alikuwa mshauri wake katika kufanya maovu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kama nyumba ya Ahabu; kwa kuwa hao walikuwa washauri wake, alipokwisha kufa babaye, hata aangamie. 2 NYA. 22:2-4 SUV.*
Umeona hapo, Ahazia alimkosea Mungu kwa ushauri mbaya wa mama yake mzazi. Unaweza kufikiri mzazi wako anaweza kukupa kitu kizuri cha kukusaidia kukujenga, kumbe anakusaidia kuvunja uhusiano wako na Mungu.
Uwe na uhakika ushauri unaopewa humkosei Mungu wako, zingatia hili siku zote za maisha yako. Maana shetani anaweza kumtumia mtu unayemwamini wewe kukuharibu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo.
Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.